Tuesday, August 21, 2012

RAIS WA LIBERIA AMSIMAMISHA KAZI MTOTO WAKE

Ellen Johnson Sirleaf anashutumiwa kwa kuendeleza upendeleo wa kindugu

Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf
Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, amemsimamisha kazi mmoja wa watoto wake wa kiume kutoka ngazi ya unaibu gavana wa benki kuu ya nchi hiyo kwa kushindwa kuorodhesha mali zake katika tume ya kuzuia rushwa nchini humo.

Charles Sirleaf, ni miongoni mwa maafisa 46 waliosimamishwa kazi kwa kosa hilo.


Ni mmoja wa watoto wake watatu wa kiume aliowateua kushika vyeo vya juu kabisa baada ya kushinda muhula wa pili wa uchaguzi mwaka jana.

Wapinzani wa Bi Sirleaf wanamshutumu kwa kuendeleza upendeleo wa kindugu.

Rais huyo amemteua mtoto wake wa kiume Fumba kuwa mkuu idara ya usalama wa taifa, na kijana mwingine Robert kuwa mshauri mkuu na mwenyekiti wa kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali-NOCAL.
Utawala bora

Robert Sirleaf anayashitaki magazeti mawili nchini humo ya Independent na Analyst, na mwanasiasa wa upinzani Jefferson Kogie kwa kumkashifu kuwa amejinufaisha kifedha kutokana na vyeo alivyopewa.

Taarifa kutoka ofisi ya Bi Sirleaf imesema Charles Sirleaf na maafisa wengine 45 wataendelea kuwa wamesimamishwa kazi hadi hapo watakapoorodhesha mali zao kwa Tume ya Kuzuia Rushwa.

Maafisa wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na mkuu wa itifaki ya rais, David Anderson, Wakili mkuu na naibu waziri wa sheria Micah Wilkins Wright na naibu mkurugenzi mkuu wa utangazaji Ledgerhood Rennie.




Liberia
Bi Sirleaf aliyeingia madarakani mwaka 2005 mwishoni mwa mgogoro wa vita Uliodumu miaka 14, amekuwa akiahidi mara kwa mara kupambana na rushwa na kustawisha utawala bora nchini Liberia.

Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka jana, muda mfupi baada ya kuchaguliwa tena kwa muhula mwingine katika uchaguzi ulioghubikwa na tuhuma za udanganyifu katika zoezi la upigaji kura.

Rushwa bado inabakia kuwa kikwazo kikubwa nchini Liberia huku idadi kubwa ya watu wakiishi katika umasikini licha ya utajiri mkubwa wa madini nchini humo.

Mwezi Juni taasisi ya kimataifa ya Maafa-ICG, ilitoa ripoti kutahadharisha kuwa rushwa na upendeleo wa kindugu katika sekta mbalimbali vinaweza kuhatarisha demokrasia nchini humo.

No comments:

Post a Comment