Mchungaji wa Kanisa la GRC, Anthony Lusekelo ‘ Mzee wa Upako’ amesema hatatoa ng’o fedha za rambirambi za Askofu Moses Kulola kutokana na kudhalilishwa kulikofanywa na wahusika wa kukusanya fedha hizo.
Akizungumza na gazeti hili Jumamosi iliyopita kwa njia ya simu, Mzee wa Upako alisema badala yake fedha hizo shilingi milioni 15 sasa zitatumika kutibu maumivu aliyoyapata kutokana na vyombo vya habari kuandika utata juu ya ahadi yake ya kutoa rambirambi hizo.
“Kwanza mimi mtu aliyetajwa kuwa angekusanya fedha hizo ambaye ni Mweka Hazina wa Kanisa la EAGT, Mchungaji Praygod Mgonja simjui kwa sura, nilishamueleza njia gani muafaka ya uwasilishaji wa fedha hizo, badala yake akatumia vyombo vya habari kunidhalilisha.
“Nilimwambia Mchungaji Mgonja kuwa shilingi milioni kumi na tano siyo kama shilingi laki tatu; Zinapaswa kuwa na utaratibu unaoeleweka wa kutolewa. Nikamwambia mama Kulola (mke wa marehemu) azifuate mwenyewe ili aniombee baraka, akasema sawa, sasa nashangaa ananidhalilisha,” alisema Mzee wa Upako.
Alisisitiza kauli yake hiyo pia kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno wa simu kwa mwandishi wa habari hii kuwa hatatoa ng’o fungu lake aliloliahidi.
Aliongeza kuwa kwa sasa ameghairi kutoa fedha hizo kwa kuwa anadhani kuna njama fulani ambazo hakuzitaja na kwamba fedha hizo sasa atazitumia kutibu majeraha aliyoyapata baada ya habari kutoka katika vyombo vya habari.
Gazeti hili wiki iliyopita lilimnukuu Mchungaji Mgonja akisema kuwa hajapokea rambirambi za Mzee wa Upako ambazo ni shilingi milioni 15 na wengine walioahidi akiwemo Mchungaji Josephat Gwajima aliyeahidi kutoa shilingi milioni 10 na Mchungaji Getrude Lwakatare (shilingi milioni moja) walishatoa.
No comments:
Post a Comment