UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa unaovuma kuelekea kambi ya upinzani, sasa unaonekana kuwaamsha viongozi wa vyama hivyo baada ya kutolewa kwa taarifa kuwa wanafikiria kusimamisha mgombea mmoja wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kabla ya kuthibitishwa na mmoja wa viongozi hao, zilieleza kuwa hatua ya vyama hivyo imekuja baada ya ushirika wao waliouunda kupinga upungufu uliokuwemo kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuzaa matunda.
Pamoja na hilo, inaelezwa kuwa maamuzi hayo magumu ya wapinzani yametiwa chachu na kauli aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete ya hivi karibuni ya kukitabiria anguko Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi wa mwaka 2015 au ule wa 2020, kutokana na kile alichodai kuwa viongozi wa chama hicho kuendekeza rushwa.
Mmoja wa viongozi wanaounda ushirika huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alithibitisha taarifa hizo huku akisisitiza kuwa nia ya kufanya hivyo ni kuhakikisha wanaiondoa madarakani CCM mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mbatia, walichokifanya kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba si nguvu ya soda na badala yake wataendeleza hadi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mbatia alisema kuwa uongozi wa vyama vya upinzani unatarajia kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja, ili kuhakikisha wanaiondoa madarakani CCM.
Mbatia ambaye alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na RAI Jumatano, alisema hatua hiyo pamoja na ushirika wao unalenga kudumisha amani na uzalendo kwa kuweka utaifa mbele.
Alisema umoja wanaoendelea kuuonyesha kwenye mchakato wa Katiba Mpya, ambao unalenga kuweka mbele maslahi ya Taifa ili kuhakikisha inapatikana Katiba bora yenye kushirikisha Watanzania wote, wataufanya pia kwenye chaguzi mbalimbali.
“Ili jambo lolote litokee lazima kuwepo na chanzo, mwanzo wetu wa ushirikiano ulioanza Septemba mwaka huu ndani ya ukumbi wa Bunge, tutauendeleza.
“Tupo kwenye maridhiano zaidi, hata muungano wetu wa Tanzania bara na Zanzibar si wa kisheria, viongozi wetu Nyerere na Mzee Karume walikaa na kuzungumza, hata sisi tunafanya hivyo, tunatakiwa kuzungumza kwa maslahi ya nchi,” alisisitiza Mbatia.
Alisema vyama vyao viliamua kuwa na ushirikiano wa pamoja kutokana na kubaini kwamba, bila umoja hakuna kitakachofanikiwa.
“Tumeshaanza kuzungumza kwa mapana juu ya ushirikiano wetu, ukweli ni kwamba kuna mwelekeo mzuri,” alisema.
Alisema hatua ya vyama kujadili kwa pamoja mchakato wa Katiba ni dalili njema za kuelekea kwenye mafanikio na ndio maana wanaona ipo haja ya kuuendeleza ushirika huo hadi kwenye chaguzi mbalimbali nchini.
“Tunapaswa kuvifanya vyama vyetu viwe vya maslahi mapana kwa taifa, ili visionekane vipo kwa ajili ya maslahi ya viongozi.
“Kwa kuwa tumeweka maslahi ya taifa mbele kwenye suala la Katiba, tumeona tuwe na mfumo ambao utalisaidia taifa, ndio maana hata tulipotoka Ikulu tumekubaliana kuwa Tanzania kwanza vyama baadaye, naamini kwa nia njema hata ule ushirikiano wetu utaendelea mbele zaidi kwa maslahi mapana ya taifa letu, tunategemea hivyo… tuna mategemeo mazuri, lazima tufikirie chanya,” alisema Mbatia.
Kauli ya Mbatia imeungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro ambaye ameeleza kuwa chama chao hakina tatizo kwenye suala la kumsimamisha mgombea mmoja na wako tayari kwa sababu ushirikiano ni suala la msingi na lenye maana.
“Kulingana na upepo wa kisiasa ulivyo sasa, ni dhahiri tunahitaji kushirikiana ili kukiondoa chama tawala madarakani, kwa sababu mahali tulipo sasa ni pagumu.
“Tunachosubiri sasa ili kukamilisha muungano wetu ni tamko la pamoja kutoka kwa viongozi wa juu wa vyama vyote, lakini naamini nia ya kusimamisha mgombea mmoja itakubalika bila kupingwa,” alisema Mtatiro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari kutoka Chadema, John Mnyika, alisema ushirikiano kwa sasa umejikita kwenye suala la kunusuru mchakato wa Katiba na kuwezesha nchi kupata Katiba bora.
Alisema ushirikiano katika masuala mengine ikiwamo pendekezo la kushirikiana katika uchaguzi, litatafakariwa kwa kuzingatia mafanikio katika ushirikiano kwenye suala la mchakato wa Katiba Mpya ambao tunaendelea nao kwa sasa.
“Huu ndio msimamo ambao naamini pia viongozi wote wanao.
“Kwa kuzingatia kauli zilizotolewa na wenyeviti wote watatu Septemba 15 mwaka huu kwenye mkutano na waandishi wa habari, wakati wa kutoa tamko la pamoja la ushirikiano,” alisema.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Dk. Benson Bana ameukosoa uamuzi huo kwa kudai kuwa hawawezi kuungana kwa sababu hawana kiwango cha kuing’oa CCM madarakani.
Dk. Bana aliweka wazi kwamba, hadhani kama vyama hivyo vitafaulu kuitoa CCM madarakani, kwa sababu havina mtaji wa kutosha wa wanachama.
Alieleza kuwa vyama vyote vitatu vinavyojiona vinaisumbua CCM, ambavyo ni CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi, havijafanya utafiti wa kutosha kubaini mtaji wa wapiga kura walio nao.
Alisema Chadema ina nguvu ndogo Bara hasa kwenye maeneo ya mijini, CUF ina nguvu Zanzibar na NCCR-Mageuzi haina nguvu ya aina yoyote jambo linaloashiria udhaifu wa vyama hivyo, ambapo alivitaka kujipa muda wa kujipanga kabla ya kufikiria kuing’oa CCM.
Wenye mtazamo tofauti na huo wanasema kuwa endapo hatua hiyo ya vyama vya upinzani itafanikiwa, ni wazi itathibitisha kauli ya Mwenyekiti wa CCM kwamba chama hicho kijiandae kung’oka mwaka 2015 au 2020.
Hata hivyo bado kuna shaka juu ya maamuzi hayo ya vyama vya upinzani, kutokana na yale ambayo yamepata kushuhudiwa katika chaguzi nyingine zilizotangulia hususani zile za viti vya ubunge.
Imeshuhudiwa katika chaguzi kadhaa vyama hivyo vikisigana kufikia maamuzi ya kuachiana maeneo ya kusimamisha wagombea wenye nguvu.
Mwaka 2010 kwenye uchaguzi Mkuu, CUF kilikitaka Chadema kutosimamisha mgombea kwenye Jimbo la Tunduru kutokana chama chao kuwa na nguvu, hata hivyo wenzao walikataa.
Hali hiyo pia ilijitokeza kwenye Jimbo la Kiteto, Chadema iliitaka CUF kutosimamisha mgombea jambo ambalo halikutekelezwa.
No comments:
Post a Comment