Na Saleh Ally
MGOGORO wa kimuziki kati ya msanii Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ na kituo kimoja cha redio umezidi kuchukua kasi huku makundi mawili, kila moja likitengeneza ngome yake na kuamini linachoamini.
Kundi ambalo linamuunga mkono Jaydee na kumuona ni mkombozi, anazungumza kwa niaba yake na wasanii wengine, la pili ni lile linalobaki upande unaoshambuliwa, linatetea ngome yake.
Jaydee anashutumu kubaniwa nyimbo zake na kituo hicho ambacho kupitia mitandao kadhaa ya kijamii ameeleza wazi kuwa wanambania, wanaziponda lakini hata watangazaji wake wamekuwa wakionyesha chuki binafsi dhidi yake.
Jaydee pia aliwaponda wasanii Ben Pol na Linah anayetokea THT kwamba walishindwa kutokea kwenye uzinduzi wa video ya wimbo wake wa Joto Hasira, kwa madai walizuiwa na bosi wao.
Ujasiri huu wa Jaydee ndiyo kitu bora ambacho kimekuwa kikitakiwa kufanyika kutoka kwa wasanii, yaani wapigane kutetea muziki wa Tanzania hasa kama kuna watu au kundi la watu limejikita katika kuuangamiza.
Lakini ni tofauti kidogo, kwani wasanii wengi wamekuwa imara na kuwa tayari kujitetea wenyewe tu na si vingine. Nasisitiza mara nyingi, wao ndiyo wahusika wa kwanza na wanapaswa kuanzisha mapinduzi kuanzia kwao, mfano kusema naonewa si kitu kibaya lakini je, umewahi kupigania wanaoonewa?
Kujitetea pekee unaweza kufanya, lakini vipi utafanikiwa kama asilimia kubwa ya kundi la wanamuziki linaendelea kuonewa. Ukibaki hauonewi pekee na asilimia kubwa ya wasanii au wanamuziki inaonewa, kunaweza kuwa na mapinduzi sahihi?
Ndiyo maana nashangazwa kusikia Jaydee leo anaona ubovu wa kituo hicho, anathubutu kusema hadharani akionyesha wazi ameumia. Lakini miaka 10 au zaidi iliyopita, Jaydee alikuwa kimya na hakuwaza kusema kwamba kituo hicho kinawabania wasanii wengine na ‘kumtukuza’ yeye hata kama muziki wake haukuwa wa kiwango kilichokuwa kinazungumzwa.
Siwezi kusema muziki wa Jaydee ni mbaya, nimekuwa kati ya mashabiki wake. Lakini yoyote atanichekesha akisema nyimbo albamu zake zote alizotoa zilikuwa katika kiwango cha juu sana na ndiyo maana leo ni maarufu.
Hakuna asiyejua kwamba miaka nenda rudi, wasanii wamekuwa wanaongoza kwa unafiki, kutopendana wenyewe, kugeukana na hata kujenga makundi lukuki, ndiyo maana kila kukicha wamekuwa wakishambuliwa maana katika maisha yao hawana umoja.
Jaydee alianza kuwa mtangazaji katika kituo hicho baada ya kuacha kurap, akaamua kuachana na kurap na mwisho kuwa msanii wa nyimbo za kubembeleza, mara ya kwanza akianza kutikisa na albamu ya Machozi, Solo Thang anaweza kuhadithia vizuri kuhusu hili.
Kuanzia albamu ya Machozi, kituo hicho ndicho kilisimama kuhakikisha anakuwa bora hata kama muziki wake haukuwa ukimzidi kila mwanadada wakati huo.
Angalia, kulikuwa wasanii kama Stara Thomas, Carola Kinasha ambao kiuwezo walikuwa juu kuliko Jaydee, lakini hawakupewa nafasi ya kutosha, badala yake Jaydee ambaye hakuthubutu kuwatetea hata kidogo akaendelea ‘kubebwa’ na watu wakaamini ni bora kuliko yoyote kwa upande wa akina dada au kina mama katika kuimba, haikuwa hivyo.
Angalia albamu ya Binti, karibu nyimbo zote zilikuwa na ujumbe mmoja, ulikuwa ukimshambulia mwaname mmoja ambaye alikuwa amemuumiza Jaydee. Takribani ujumbe wa nyimbo karibu zote ulikuwa ni mmoja, lakini ilibebwa na kuonekana ni moja ya albamu bora kabisa kuwahi kuwepo katika muziki wa Tanzania, kitu ambacho hakikuwa sahihi.
Wakati huo wasanii lukuki walilia kubaniwa, mmoja wao alikuwa ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ndiye alimtambulisha mwanadada huyo alipomshirikisha katika wimbo wa Mambo ya Fedha, kabla ya hapo hakuwa na jina. Jaydee hakuwahi kuungana naye hata kidogo hata kwa mstari mmoja wa kumtetea au kuunga mkono kutetea muziki wa Tanzania, kuonyesha anapinga mwenendo wa wanaolazimisha kuwabagua wasanii au kufanya mambo kwa mabavu kwa kuwa wameshika mpini.
Hakuna aliyesikia kilio cha Sugu, wasanii wanaochipukia bila ya kujua wasemacho, kisa nyimbo zao zinapigwa redioni, ili kuonyesha shukrani za dhati wakaanza kutangaza Sugu anatapatapa na amekwisha kimuziki!
Ajabu, asilimia kubwa ya maneno yake ndiyo yanayozungumzwa leo, ndiyo yanatumiwa na kila msanii anayebanwa au kuhisi kaonewa. Angalia, hata Jaydee naye ameingia huko! Swali langu hapa je, Jaydee na wengine wanaolalamika, wamekwisha kisanii?
Ndiyo maana nasema, tasnia ya muziki hasa muziki wa kizazi kipya umejaza watu wavivu kufikiri, wenye mioyo ya ‘Kichina’, wasio na uwezo wa kuthubutu hata kidogo ambao wanasubiri wayumbe au kuumizwa wao ili wamtafute wa kumuangushia lawama.
Jiulize, kama Jaydee alibebwa kwa miaka 10, halafu leo analalamika atakuwa sahihi? Sitaki kumpinga kwa kuwa kuna kitu anakiona lakini ninaamini alikiona tokea mapema, akauchuna.
Bado nasisitiza, yeye na wengine wote wanaolia baada ya kuguswa wao nawaita wanafiki, wanapigana kwa ajili yao na si kwa muziki wanaoutumikia. Iwapo wangekuwa tayari kupambana kwa ajili ya muziki huo, msanii kama Jaydee asingeanza vita leo.
NARUDI KWA JAYDEE
Sijawahi kuingia naye katika malumbano zaidi ya miaka 10 tokea alipokuwa mwanahabari mwenzangu na sasa msanii. Lakini nathubutu kumueleza kuwa ni kati ya wasanii wasiojali muziki wa Tanzania na wanajiangalia wao zaidi.
Picha ya unafiki na kujiangalia mwenyewe inaonekana sasa ingawa takribani miaka mitano iliyopita nilianza kuinusa. Leo analia, anabaniwa na anauona moto unaounguza muziki wa Tanzania ulivyo mkali.
Naamini aliuona miaka kibao nyuma, lakini kwa kuwa alikuwa akitetewa hakuweza kuangalia kwamba rafiki zake, wasanii waliombeba kabla walikuwa wakiungua. Akaendelea kuwapita kwa raha zake mustarehe.
Tungeweza kumuita Jaydee ni mpambanaji kama angewakosoa hao anawakosoa sasa katika kipindi walichokuwa wamempa mbeleko yeye, basi kweli ingeonekana anapigania muziki wa Tanzania. Sasa anapigania chake tu!
Jaydee amefika mbali kimuziki, alikuwa bora jukwaani na nyimbo kadhaa na nyingi zikapewa ‘over promotion’ lakini bado ninaweza kumuita mkongwe. Ajabu alibaki chipukizi hadi leo katika suala la kutetea haki za wasanii na muziki wenyewe.
Sitaki kumkatisha tamaa kwa mapambano aliyoyaanza, ninaamini ana nafasi ya kuanza kuusaidia muziki ambao umemsaidia. Lakini ndiyo kipindi ambacho anaweza kupata machungu waliyopata wasanii wenzake kunyeshewa mvua na kuunguzwa na jua wakati akiwa kivulini kwa ‘msaada’.
Anachokifanya leo Jaydee ni nyongeza tu ya walichokifanya Sugu au Afande Sele au wasanii wachache walioamua kuwa wakweli au wale walioamua kuwa wabunifu kama Ambwene Yessaya ‘AY’, aliyekimbia vita ya redio na kuingia katika kurekodi video bora zilizoendelea kumng’arisha.
Simzuii, Jaydee kuendelea kupambana, lakini namuasa anachokifanya kama ni kwa ajili ya muziki akipozwa tena, asirudi nyuma.
Ninachomkumbusha, hata yeye amekuwa kundi moja na analowalaumu ambao angeweza kuwashauri mapema ‘ndani ya mjengo’ kama angekuwa na nia nzuri na muziki wa kizazi kipya. Msisitizo ‘Joto Hasira’ liwe la kweli.
No comments:
Post a Comment