Wednesday, June 17, 2009








---------------------------------------------------------------------------


Wasomaji, naanza na BAPisms:

Ø
Maisha bora hayanyeshi kama mvua; sio tukio (event)! Maisha bora ni mchecheto (process) yanatokea baada ya muda (over time).

Ø Wakati mwingine ni vigumu kuwabadilisha walalahoi wetu; inabidi twende pole pole na baadhi ya walalahoi wetu wanaolegalega (the laggards) ili tufanikiwe kuwavusha.

Ø Wa-Barbaig ni wa-Tanzania wetu; tuwatoe kutoka hizo nyumba zao za jadi hadi kwenye nyumba za kisasa zenye matofali ya udongo na kuezekwa kwa nyasi.

Ø Tunaweza kuboresha nyumba za tembe za wa-Gogo za asilia (nyumba zinazolinga na mazingira) kwa kuziwekea madirisha na milango ya kisasa hata kuwa nyumba za maghorofa-tembe!

Ø Tuwavushe wa-Jita wangu wote kutoka hizo nyumba zao za udongo zisizo na madirisha (eti, wanaogopa wachawi watawachungulia usiku.)

Ø “Nyumba bora sio lazima ijengwe kwa matofali ya kuchoma na kuezekwa kwa bati. Kuna magofu ya majumba ya zamani yaliyozagaa kwenye “amatongo” (mahame) huko kwetu (Majita, Musoma) yaliyojengwa kwa matofali mabichi ambayo bado yamesimama baada ya kuwa “oxidized” na jua!

Ø Magofu ya namna hiyo (adobe houses) pia yapo sehemu za mikoa ya Arizona na New Mexico hapa Amerika ya wazawa wa nchi hii.

BAPisms hizo zinatokana na Maggid Mjengwa kuweka kwenye blog yake (mjengwa.blogspot.com) picha yenye kichwa, “Maisha Haya ' SI MCHEZO!'... Hata Kama....”, ikionesha watoto wetu huko vijijini wakijisomea gazeti la Si Mchezo nyumbani kwao.

Akichangia, anonymous wa tarehe: 30/9/08 1:01 PM aligusia jambo moja muhimu, ambalo lilinikuna akili, pia:

“HIZI NYUMBA ZA NYASI ZITAKWISHA LINI VIJIJINI, JAMANI, na hawa watoto wetu nao wa(si)kulie katika mazingira yaleyale ya akina Zinjanthropus? No, this is not acceptable. Hata kama nyumba zote hazitaezekwa kwa bati, lakini angalau basi hata ujenzi wa kuta zenyewe za nyumba zionyeshe dalili ya uhai kidogo.
“Mazoea ni kitu kibaya. Wanasiasa wetu hodari sana kwa kuomba omba misaada. Wanangoja nini kuwaelimisha hao wanavijiji wetu angalau hata teknolojia asili ya kufyatua matofali na kuyachoma na kisha kujenga nyumba za kisasa kulingana na uwezo uliopo pale kijijini? Makazi Bora kwanza ndipo Kilimo cha Kisasa kisha Elimu Bora ikifuata Afya ya Kinga na hatimaye Viwanda na Maendeleo zaidi huko vijijini!
“Mjengwa, unasemaje kuhusu hilo? Huwa inanitia uchungu sana karibu nchi nzima kila uendako vijijini karibu asilimia 96% ya nyumba zote za makazi ya watu ni za nyasi tupu! Nyumba za Bati na Matofali ni za kubahatisha tu. Mafanikio ya wanasiasa wetu ni nini basi? Kutuwekea viwanda vinavyotengeneza bia nusu lita ikauzwe kwa shilingi 1,200/= au zaidi? Kupata maji safi na salama huko vijijini ni sawa na kuwa na mgodi wa dhahabu? Where are heading to?”
Wa-Tanzania wengi wameona hiyo picha niliyoweka hapo juu (Rais Bwana Jakaya Mrisho Kikwete akitoka katika nyumba moja ya m-Barbaig alipokitembelea Mkoa wa Manyara hivi majuzi).

Katika picha hii, msaidizi wa Rais anainua nyasi zisiingie katika nywele za Rais wetu au kumchoma kichwani au kumwingia machoni. Ni matumaini yangu kwamba kwa wakaaji wa nyumba hiyo bughudha ya nyasi hizo yaiwaletei “msongo na mavune”; ni kitu cha kawaida tu!

Uzuri wa picha hii au niseme ujumbe wake una maana kubwa. Hapa hatumwoni Rais wetu akiingia ndani ya nyumba hiyo! Wala hatumwoni Rais wetu akiwa ndani ya nyumba hiyo! Wala hatujui katumia muda gani akiwa ndani ya nyumba hiyo! Tunamwona Rais wetu akitoka nje kwa kuinama.

Si ajabu mgongo wa Rais wetu uliuma kwa kuinama! Si ajabu magoti ya Rais wetu yaliuma kwa kuinama! Si ajabu Rais wetu kasema kimoyomoyo, “Uongozi una taabu”! Si ajabu Rais wetu kasema kimoyomoyo, “Kamwe sitaingia nyumba ya namna hii tena”!

Hata tukisahau niyoandika hapo juu, ukweli utabakia pale pale kuwa Rais wetu kaguswa na hali halisi ya maisha ya wananchi wetu wanaoishi katika nyumba hiyo, hasa, na wale walalahoi wengine wenye maisha ya namna hiyo popote pale Tanzania, kwa ujumla! Rais wetu kayaonja maisha ya ki-lalahoi!

Mosi, Rais wetu hana budi kuutafsiri huo “msongo na mavune” yaliyomsibu kwa kuiangalia hiyo nyumba ya m-Tanzania wake kabla ya kukaribishwa au kujikaribisha ndani.

Pili, Rais wetu hana budi kuutafsiri huo “msongo na mavune” yaliyomsibu alikiingia ndani.

Tatu, Rais hana budi kuutafsiri huo “msongo na mavune” yaliyomsibu akiwa ndani amechuchumaa, amesimama ama amekaa!

Nne, Rais hana budi kuutafsiri huo “msongo na mavune” yaliyomsibu akitoka nje ya nyumba hiyo!

Kama kweli Rais wetu kaguswa na “msongo na mavune” hayo, ajue kuwa hiyo ni nyumba na maisha ya m-Tanzania (au wa-Tanzania) waliopiga kura katika uchaguzi uliopita. Si ajabu walikipigia Chama cha CCM na kumpigia mgombea wake Jakaya Mrisho Kikwete awe Rais wa Tanzania!

Rais wetu hana budi kuutafsiri huo “msongo na mavune” kutokana na ahadi yake kwa wa-Tanzania wa namna hiyo waliomsikia akiwika Bungeni (Desemba 30, 2005): “Maisha Bora kwa Wote”!

Kama kweli kaguswa na hali halisi ya maisha ya namna hiyo, angalau kwa dakika sijui ngapi alizotumia humo ndani ya nyumba hiyo, nachukua nafasi hii kumwomba Rais wetu aungane na wasomaji wengine, na wote warejee makala na hoja za dhati zinazojitokeza za mwandishi Joseph Mihangwa, Wabunge Wanapolilia Mkia wa Kondoo” (Toleo Na. 049) la Raia Mwema (au http://raiamwema.co.tz/).

Mengi yameandikwa hivi karibuni juu ya kero hii, kama Mbunge Wilbord Slaa (Karatu-Chadema) alivyolitaadhari taifa juu ya w a-Bunge kujiongezea mapesa! Na bila kusahau kuibiwa kwa u-wazi na makusudi kwa fedha za umma katika BoT na wale wote waliotoa siri kwa hao wezi kuwakaribisha na kufanikisha wizi huo!kuiba hizo,

Ningependa Rais wetu, Bwana Jakaya Mrisho Kikwete, na wa-Bunge wake, ikiwa ni pamoja na viongozi wa mihimili mingine muhimu ya serikali, waahidi na kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya “NEVER AGAIN” ku- “acquiesce” na maisha duni ya namna hii! Yaani, tutoke nje ya mazingira ya namna hii, kama Rais wetu anavyotoka nje ya nyumba hiyo!

Lakini cha ajabu ni kwamba picha, kama hizi, huwa tunapenda kuziangalia tu na wakati mwingine kuziondoa upesi, upesi machoni mwetu (sisi wenye uhondo wa ulalaheri) bila kuzitafakari kwa nia ya kuleta maendeleo nchini kwa wale wenzetu ambao wanazidi kukandamizwa na ualalahoi.

Tusiimbe au tusilaani tu kaulimbiu za “Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya”, “Maisha Bora kwa Wote” au “Maisha Bongo ni Tambarare”! Swali la changamoto kwa wote: Je, nyumba ya namna hiyo tunawezaje kuibadilisha iwe ya kisasa?

Hebu twende na mabadiliko ya nyumba hii, huku tukizingatia kwamba mabadiliko ya nyumba hii ni mabadiliko ya wakaaji wake, pia!

Naendeleza hoja yake: Nyumba hiyo iifanyiwe “make-over” ya kujengwa kwa matofali mabichi. Isiezekwe kwa bati, bali kwa nyasi ili kukinga joto na mvua. Ikiezekwa kwa bati, itakuwa tanuru wakati wa jua kali. Bila dari, wakati wa mvua ya mawe, itakuwa mlio wa bunduki; usiku hakuna kulala!

Tuanze kutumia akili zetu, polepole. Hayo ya “ari mpya, nguvu mpya, kasi mpya” yasiwe tu maneno ya ki-siasa: maneno matamu; ahadi tamu za kupata kura tuingie Ikulu, u-Bunge, u- Wakilishi wa Serikali za Mitaa au tupate kazi huku tukiwasahau wakulima, wavuvi. wachungaji, wawindaji mwiruni, waokotaji mwituni!

Tukiacha maisha yaende kwa ndoto zake za ki-“evolution”, itatuchukua pengine karne nyingi kuweza kubadilika kutoka nyumba ya kwanza kwenda nyumba ya pili, kama zinavyoonyeshwa hapo chini.

Lakini tunaweza, kwa akili zetu za leo, kabisa tukavuka hizo karne kwa kuingilia kati (to purposefully intervene) na kubadilisha nyumba, kama hiyo anayotoka Rais wetu Bwana Jakaya Mrisho Kikwete huko kwa wa-Barbaig.

Tutoke kabisa katika nyumba ya namna hiyo na tuingie, angalau, nyumba kama hizo za juu:

Nyumba hiyo izidi kufanyiwa “make-over”. Tunazo nyumba nyingi zilizofikia hali hii, ambazo hazina budi zifanyiwe “make-over”, pia, kwa kuweka milango, na madirisha hata ya vioo na mapazia, kama ilivyo mifano ya nyumba hizi zilizoko kwenye picha hapo juu ;

Tuzidi kupiga hatua kwenda mbele na kuweka umeme (uzalishwao na maji, mionzi ya jua au upepo) na gesi ya kupikia, endapo wenye gesi hawataiuza kwa nchi za nje hata kabla ya kukidhi mahitaji ya wa-Tanzania. Si gesi ni yao 75%; wanailipa Tanzania “royalties” na gesi itauzwa, kwa mfano, Kenya!

La sivyo, bila kuwaelekeza wa-Barbaig itawachukua tena karne kumi kuweza kubadilika, ama wasibadilike kabisa!

Kwa vyovyote vile, tunaweza tukafanya mapinduzi ya kutoka nyumba picha ya kwanza kwenda picha ya tatu bila kupitia kwa “mkunga-nyumba” (mid-wife) picha ya pili!

Lakini huenda mapinduzi ya namna hiyo yakawa ni makubwa sana kwa wa-Barbaing na walalahoi wetu wengine! Tutawafanya waathirike “na msongo na mavune” (stress and strain) au kwa lugha nyingine, “future shock” shauri ya kufika kwa “vya usasa” ambayo hatukujitayarisha kuvipokea (the sudden arrival of the future for which they are not prepared)!

Huku tukiandaa maisha yao yaende sambamba na mabadiliko ya nyumba zao, yatubidi twende na baadhi ya walalahoi wetu wengine pole pole, hasa wale wanaolegalega (the laggards) ili tufanikiwe kuwavusha.

Kwa kifupi, tunaweza kabisa kubadilisha maisha (utamaduni wa nyumba bora na mazingira) ya walalahoi wetu pole pole kwa kuanza na wale wapendao. Na baada ya miaka ishirini hivi, mazingira yetu huko vijijini yatabadilika kabisa na kuwa ya “usasa”! Hii haina budi kuwa sera ya maendeleo na wala si ya ki-siasa

Na kwa wa-Tanzania wengine wa vijijini, achaneni na nyumba za bati (kama hamna pesa za kununulia hayo bati). Jengeni na ezekeni kwa nyasi! Tumieni hizo pesa za mabati kununulia samani na mahitaji mengine ya lazima! Cha kujihadhari ni moto kwa nyumba zetu hizo zilizoezekwa kwa nyasi!

Angalieni mifano ya picha za nyumba tano za namna hiyo hapa juu:

Wakati akianza kazi ya u-Rais, Bwana Jakaya M. Kikwete aliahidi kuboresha ajira kwa vijana wetu kiasi cha milioni moja kila mwaka. Sawa. Lakini ahadi ni deni!

Tunaweza kabisa kukidhi na kuzidi kuwapatia ajira-manufaa (functional employment) kwa vijana wa Tanzania, huku wakishiriki katika mchakato wa kuboresha maisha ya walalahoi vijijini.

Sababu ya kutaka kutoa ajira-manufaa tunayo. Kinachokosekana ni uongozi (akili) wa ki-siasa. Na ahii inatokana kwa sababau viongozi wetu wengi wanashughulika kutengeneza “fweza” kutokana na michakato ya u-binafsi, kiasi cha kukosa nafasi au kutumia akili zao za uongozi kwa vya umma!

Kuna haja ya kujenga "brigedi" za vijana wasio na kazi, ki-mikoa, ki-wilaya na ki-tarafa: brigedi za kufyatua matofali (ikiwezekana ya kuchoma – sio lazima); kujenga nyumba; brigedi za useremala na utengenezaji wa samani za nyumbani; au brigedi za ushoni (ikiwa ni pamoja na magodoro ya kukalia na kulalia na mapazia na kufuma mazulia kwa katani na makuti na ukindu! Mapesa ya JK yamwagwe huko!

Huenda tukafanikiwa kubadilisha mitindo mazingira ya wana-vijijini (pamoja na maisha ya walalahoi wetu). Hii italeta nyumba bora vjijini pamoja na kuchangia maisha bora kwa wote. Miktadha ya hizo nyumba ni lazima iendane na mabadiliko ya akili, usafi wa mazingira, na vitu vya kutumia nyumbani.

Kuweza kuleta maisha bora kwa wa-Tanzania wetu ni lazima tupambane kuyaboresha kwa kutumia mbinu zote za vita hii. Vita yenyewe ni “frontal” –pande zote za mstakabali wa binadamu!









Barua pepe: romuinja@yahoo.com

No comments:

Post a Comment