Tuesday, May 22, 2012

NENO FUPI LA USIKU HUU NA JOHN CHIBUDA

Ndugu zangu,

Mtanzania mwenzetu John Shibuda ameibua hoja ya ukabila. Nakubaliana na John Shibuda kwenye hoja ya kutaka haki yake ya kutangaza nia ya kuwania Urais wa nchi hii iheshimiwe. 

Shibuda ana haki hiyo. Na haitakuwa mara ya kwanza kwake kututangazia Watanzania nia yake hiyo.
Lakini, inasikitisha, kuwa hoja ya pili ya John Shibuda imechangia kuua hoja yake ya kwanza; ni hoja ya ukabila. 

Shibuda anaonekana kututaka Watanzania tujadili ukabila na hususan chama chake cha Chadema na ukabila ulio ndani ya chama hicho.

John Shibuda ni mmoja wa viongozi ninaowaheshimu sana kwa mchango wao kwa taifa letu. Naamini, kuwa John Shibuda anaheshimika na wengi wengine hapa nchini. Lakini, kwa kutuletea hoja ya Chadema na ukabila,  nahofia John Shibuda amepotea.  

Hoja yake haina msingi. Imejengeka katika hisia kuliko uhalisia. Yumkini, John Shibuda amekuja na hoja hii sasa, ama , kwa bahati mbaya, au kukusudia. Hilo la mwisho halina kusudi la kujenga, bali kubomoa. Inasikitisha.

Maana, hoja ya ukabila haina umaarufu katika nchi yetu kwa sasa. Watanzania wa sasa hatuendekezi ukabila. Kauli ya Shibuda kuwa anabaguliwa katika chama chake cha Chadema  kwa vile ni Msukuma haikupaswa kutamkwa kwa mtu kama Shibuda.  Na haikupaswa kutamkwa na yeye na bado akaendelea kubaki katika chama anachoamini kina ubaguzi wa kikabila na huku yeye mwenyewe akiwa muathirika wa ubaguzi huo.

Na kwa vile hana ushahidi wowote wa kuthibitisha anachosema, Shibuda anachochea moto ambao Watanzania hatuutaki. Ukabila ni moto wa hatari, kama ilivyo kwa moto wa udini.

Kama Shibuda analalamika kuwa anabaguliwa kwa vile ni Msukuma, ingekuwaje basi, John Shibuda angeitwa Ramadhan Shibuda? Je, angeongeza dai la pili; kuwa anabaguliwa Chadema kwa vile ni Muislamu. Si Mkatoliki?

Kama John Shibuda anadhani kauli zake za ukabila zinakisaidia Chama chake cha zamani cha CCM, basi, napo anakosea; maana, kwa CCM kuhusishwa sasa na kauli za Shibuda za ukabila, kunakiharibia zaidi CCM kuliko kukijenga kwa Watanzania walio wengi.  Lililo bora kwa CCM sasa ni kujitenga na kauli za Shibuda juu ya ukabila . Maana, Watanzania wa leo si wa jana.  Ni wepesi sasa wa kubaini hila na ghilba za wanasiasa. Wengi wanaonekana kusikitishwa na hoja ya John Shibuda juu ya kubaguliwa kwa vile ni Msukuma.  Wanasikitika kwa vile wanadhani hoja imejengeka katika hila na ghilba kwa wananchi.

John Shibuda afahamu ukweli huu;  Watanzania walio wengi  kwa sasa wanataka mabadiliko. Wanaiona sasa mishale ya saa ya mabadiliko ikisonga mbele. Wanamwona hata Rais wao, Jakaya Kikwete akisaidia kusukuma mabadiliko hayo.Ni mabadiliko ya kimfumo. Ni wangapi walifahamu kuhusu uwepo wa CAG miaka mitatu iliyopita?  Upinzani bungeni, ndani ya chama tawala, na uwepo wa ofisi ya CAG iliyopewa nguvu umeanza kurudisha matumaini ya Watanzania.

Naam, Watanzania hawataki tena kurudi katika mfumo wa Chama kimoja  kilichoshika hatamu. Majaribio yote ya kuua upinzani, kufuta fikra huru, yatazidi kulaaniwa na walio wengi katika nchi hii.

Hivyo, John Shibuda hawezi tena leo kurudisha nyuma mshale wa saa ya mabadiliko; hata kwa ajenda ya ukabila. Na hili ni Neno Fupi la Usiku Huu.

Maggid Mjengwa,
Kigoma.
0788 111 765



No comments:

Post a Comment