Tuesday, June 5, 2012


Historia inaonyesha kwamba wanamuziki wengi hupitia vikwazo vingi mpaka kufikia mafanikio. Ni hali halisi ambayo bila shaka inaeleweka ukizingatia utitiri wa vijana wenye vipaji vya kuimba na hata kutunga au kuandika nyimbo. Wapo wengi.Katika sanaa ya muziki kuna kukataliwa, kuna kuambiwa huwezi, hujui kitu na huwezi kufika mbali.
Pamoja na ukweli huo, kuamua kuendelea au kukubaliana na “maoni” ya wadau na kuachana na muziki, kunategemea mambo kadhaa ikiwemo imani binafsi kama unaweza au huwezi. Ukiambiwa huwezi na wewe ukakubaliana na hoja hiyo,bila shaka utakuwa umefikia mwisho wa ndoto.Unaamka.
Lameck Ditto ni miongoni mwa wanamuziki ambao wamepitia vikwazo vingi mpaka kufikia hapo alipo hivi leo. Bila shaka tunakubaliana kwamba Ditto ni miongoni mwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya wenye vipaji, nidhamu na juhudi za hali ya juu katika sanaa ya muziki.
Kufikia hapo alipo, alipitia mengi. Alistahimili mengi. Aliwahi kuambiwa hawezi. Aliwahi kutembea kwa mguu masafa marefu ili kwenda studio kwa sababu mfukoni hakuwa na nauli hata ya daladala. Kukaja masuala binafsi ya kufiwa na Mama yake mzazi akiwa bado kijana mdogo tu. Kwa muda mrefu hakumjua baba yake. Akaishi kwa kubahatisha kama vile mtoto wa mtaani. Pamoja na yote hayo,akaendelea kuamini kwamba anaweza na sanaa ndio itakayomtoa. Kama alivyoimba katika wimbo wake “Tushukuru Kwa Yote”, Ditto akaendelea kushukuru na sasa anaanza kuonja mafanikio ya uvumilivu;
Nini kinamfanya kamwe asikate tamaa? Baada ya kufikia mafanikio ambayo anayo hivi sasa,ana mipango gani? Ilikuwaje akaamua kwamba sanaa ya muziki ndio uwanja wake wa kujidai? Fuatana nami katika mahojiano yangu na Lameck Ditto, akielezea kule alikotoka,alipo na anapotaraji kufika na mengine mengi;

BC: Hello Ditto,karibu sana ndani ya BC.Tunafurahi kuwa nawe hivi leo.Labda kwa haraka na kwa faida ya msomaji ambaye hakufahamu, unajielezeaje? Ditto ni nani.Ni mtu wa aina gani?

LD: Asante sana Jeff.Nami nafurahi sana kuwa nawe ndani ya BC. By the way unafanya kazi nzuri sana.
Kwa kifupi tu Ditto ni mwimbaji na mwandishi wa nyimbo. Ni kijana ambaye anajitahidi kujituma katika shughuli zake yeye binafsi na pia kutoa msaada katika shughuli za wenzake kila anapohitajika na kila inapowezekana. Ni kijana mwenye imani katika kufanikiwa bila kujali chochote kinachohusiana na ugumu wa kufanikisha jambo.Ni mpole,mcheshi,msikivu na anayependa kujiendeleza.Huyo ndio Ditto.

BC: Mara nyingi wasanii huanza kupenda aina fulani ya muziki kutokana na waimbaji au wanamuziki walioanza kuwasikiliza tangu wakiwa watoto.Kwa upande wako unakumbuka ulipenda kusikiliza miziki ya kina nani au bendi gani? Unadhani miziki hiyo ilichangia katika uamuzi wako wa kufanya aina ya muziki unaofanya hivi leo?


LD: Kama kijana mwingine yeyote, nilipenda kusikiliza muziki. Na hata nisingependa wakati nazaliwa televisheni zilikuwa bado sio maarufu kwa hiyo nyumbani ukiingia utakachosikia ni redio na mara nyingi redio na muziki na mtu na nduguye. Kwa hiyo niliwasikiliza wanamuziki wengi.
Lakini ambao naweza kusema walinivutia zaidi ni wanamuziki kama vile Hayati Marijani Rajabu kwa upande wa wanamuziki wa kizazi cha awali na watu kama Banana Zorro,Lady jaydee Na Prof J kwa upande wa wale wa kizazi kipya..

BC: Katika tovuti yako,historia inaonyesha kwamba wewe ni pacha.Pacha wako(Kulwa kama sikosei) naye anafanya muziki? Una ndugu mwingine yeyote anayefuata nyayo zako katika muziki?

LD: Ni kweli mimi ni Dotto na nina mwenzangu ambaye ni Kulwa kama ulivyobainisha. Kwa bahati nzuri au mbaya, Kulwa yeye hana mapenzi makubwa na kuimba japokuwa ana kipaji kikubwa sana. Huwa nikimsikia anapoimba baadhi ya mashairi ya nyimbo zangu, kwa mfano, huwa najiona mimi nasubiri kabisa kwake. Hakuna ndugu yangu mwingine anayeimba.Kama yupo basi hatufahamiani.Unajua tena dunia uwanja mpana sana huu.


BC: Mbali na muziki, umewahi kufanya kazi nyingine yeyote kwa minajili ya kujipatia kipato au riziki?

LD: Hapo kabla nilijaribu kuwa fundi makenika. Muziki ukanitoa huko. Pia nimewahi kujishughulisha na biashara ndogo ndogo kitu ambacho nimekiendeleza mpaka leo.Na hivi karibuni kuna kampuni yangu binafsi itaanza kazi…itafanya nini? Vumilieni kidogo.Wote mtajua.

BC: Kwa muda mrefu ulikua bila kuwa na mahusiano na baba yako mzazi. Historia yako inaonyesha kwamba kwa mara ya kwanza mlikutana katika msiba wa Mama yako(Mwenyezi Mungu aendelee kumpumzisha kwa amani). Mahusiano yako na baba yako yakoje hivi sasa? Maisha yalikuwaje kukua katika malezi ya mzazi mmoja? Na una ushauri gani kwa wengine ambao, kwa sababu moja au nyingine,hawapo karibu na wazazi wao?

LD: Ni kweli kabisa Jeff kwamba mara ya kwanza kuonana na baba yangu mzazi ilikuwa katika msiba wa mama. Baada ya hapo tumeendelea kuwa na mahusiano ya baba na mwana.
Malezi ya Baba na Mama ni jambo la msingi sana kwa mtoto. Kukua katika mkono wa mzazi mmoja kuna changamoto kubwa sana hususani katika kujenga msingi wa maisha ya mtoto. Lakini namshukuru sana Mama yangu alijitahidi sana. Amenifanya naishi katika msingi alionitengenezea. Kwangu mimi, yeye ni shujaa. Kila siku najisikia imara nikimkumbuka.
Ushauri kwa vijana wenzangu, tuwalee watoto wetu ili tujenge kizazi imara.

BC: Ipo imani kwamba ili msanii atambulike ipasavyo na apate mafanikio,basi mahali pazuri ni Dar-es-salaam. Wewe ni mfano wa wasanii ambao kwanza mlikuwa mkoani(Morogoro) na kisha mkahamia Dar na kama tunavyokuona,una mafanikio mazuri.Unazungumziaje suala au imani hiyo?Ni kweli?Kwanini?

LD: Imani hiyo ipo na inaweza kuwa na ukweli. Kwa mfano, ni ukweli kwamba studio nyingi zipo Dar-es-salaam.Vituo vingi vya radio vinavyotamba nchini vipo Dar-es-salaam. Vituo vya televisheni pia na hata wadau wa muziki kwa ujumla. Lakini hiyo sio kusema kwamba hakuna vipaji ambavyo vinaweza vikapikwa mikoani na kutamba. Mifano ipo ya wasanii ambao wanafanya vizuri mikoani japo nao kwa njia moja au nyingine hufikia mahali ikabidi wajihusishe na Dar-es-salaam!

BC: Mbali ya kuimba,wewe pia ni mtunzi na mwandishi mzuri wa nyimbo.Umeshaandika nyimbo kama Darubini Kali uliyoshiriki ukiwa na Afande Sele na nyimbo kama Kariakoo ya Mataluma. Niambie kidogo kuhusu mlolongo wako mzima wa kuandika wimbo.Nini huwa kinaanza na kipi kinafuata mpaka wimbo unapokamilika?

LD: Asante kwa sifa hizo. Lakini wimbo Darubini sikuandika mimi japokuwa nimeishiriki kwa kiasi kikubwa. Katika utunzi kinachoanza ni wazo la wimbo. Kisha kinafuata mtindo wa kuandika kutegemea na aina ya muziki wa huyo unayetaka kumuandikia. Kisha baada ya hapo mabadiliko hutokea au huenda sambamba na jinsi matayarisho yanavyoanza mpaka kufikia mwisho..

BC: Wimbo wako wa Tushukuru Kwa Yote, ulipamba moto wakati Tanzania ilikuwa inasheherekea miaka 50 ya Uhuru. Kukawa na maneno na mitizamo tofauti.Wengine wakasema tushukuru kwa kipi? Wengine wakasema tushukuru kwa amani na vitu kama hivyo.Ulivyokuwa unauandika nini hasa kilikuwa kichwani kwako?Unajisikiaje kuona kwamba kile ulichokiandika kinaleta gumzo la hapa na pale?

LD: ah aha aha kama msanii, kitu kama hicho kinapotokea huwa naona ni nimefanya kazi yangu vizuri maana yake nimetimiza wajibu wangu.Mimi niliutunga kichwani nilikuwa napata picha ya kitu au watu ambao wanatakiwa kuwa pamoja bila kujali magumu wanayopitia.Sikuutunga kwa ajili ya sherehe za uhuru .Isipokuwa kwa sababu ulitoka kipindi kile watu wakaona waaunganishe na uhuru. Bahati nzuri ni kwamba hadi sasa umekuwa kila linapotokea tukio ni Tushukuru kwa Yote.

BC: Mambo mengi sana yamesemwa kuhusu T.H.T. Mengine mazuri na mengine mabaya.Bila shaka umeshasikia.Tukichagua kuongelea yale mazuri, unadhani T.H.T imekusaidiaje wewe binafsi kama msanii.Ni mambo gani ambayo unadhani usingepata nafasi ya kuwepo pale T.H.T pengine usingejifunza au usingekaa ukayajua?Kivipi?

LD: Ni kweli kwamba mengi huwa yanasemwa kuhusu T.H.T…sasa bila kuingia katika hayo malumbano, ninachoweza kufanya hapa ni kukueleza yale ambayo, kama ulivyoshauri katika swali lako, nimefaidika nayo tangu niende T.H.T. Leo hii mimi kama msanii naweza kusimama popote ndani na nje na nikaimba na watu wakanielewa. Naongelea kuimba katika Live Band.Nimekaa katika misingi ya uimbaji. Nimeweza kuutambulisha muziki wangu tofauti na hata mimi nilivyotarajia. Leo hii nikiimba jukwaani naimba na watu neno hadi neno.Maisha pia yanaenda.Isitoshe nafurahia maisha yangu hapa na ninaamini kila nilichokuwa naota kinaenda kutimia.

BC: Kwa mtu yeyote ambaye amepata nafasi ya kujua mawili matatu kuhusu historia yako, nina uhakika atatambua kwamba umepitia mambo mengi magumu na ingekuwa rahisi sana kukata tama. Ni kitu gani,kile cha ndani hasa,ambacho kimekuwezesha kuendelea na kutokata tamaa?

LD: Brother Jeff, mimi naamini kabisa moyoni na mwilini kwangu kwamba nimeumbwa na neno la kutoshindwa.

BC: Umeanza kuimba ukiwa na umri mdogo tu.Mbali na kuimba pia wewe ni mpenzi mkubwa wa mpira wa miguu(soka) na umewahi kusema kwamba usingekuwa mwimbaji ungependa kuwa mwanasoka ingawa unakiri kwamba kiwango chako katika soka ni kidogo sana.Unazipenda timu gani za soka hapa nchini na duniani kote? Na mbali ya muziki na soka(naamini at least unapenda kuangalia), unapendelea kufanya mambo gani mengine unapokuwa na muda?

LD: Kwa upande wa hapa nyumbani mimi Ni Shabiki Wa Simba na katika soka la kimataifa mimi ni shabiki wa Manchester United. Ninapopata muda wa ziada napenda kupumzika na marafiki nyumbani kwangu na kubadilishana mawazo.

BC: Kama ningekupa offer ya chakula cha jioni,ungependelea kula chakula gani? Na wakati wa chakula hicho ingewezekana ungependa kuwaalika watu gani watatu(hai au waliofariki)
LD: January Makamba,Zitto Kabwe Na Marehemu Amina Chifupa.


BC: Naamini kabisa kwamba unapenda sana kusikiliza muziki au nyimbo za watu wengine.Katika kusikiliza kwako,ni nyimbo gani au zipi ambazo huwa unatamani kwamba ungekuwa wewe ndio mwandishi wake?

LD: My Hope is In You ya Youssou Nd’our, Chuki Ya Wayre, Machoni Kama Watu ya AY na Nyimbo karibia zote za Lokua Kanza.

BC: Nini malengo yako katika miaka 5 ijayo? Na una ujumbe gani kwa mashabiki wako? Wajiandae na nini kipya kutoka kwako mwaka huu?

LD: Mashabiki wangu waendelee kutegemea muziki mzuri kutoka kwangu.Malengo yangu baada ya miaka mitano ni kuwa na nguvu kubwa kimuziki wa Africa na dunia nzima.

BC: Asante sana kwa muda wako Ditto. Shukrani

LD: Asante na wewe endelea kutangaza wanamuziki wa Tanzania na East africa Yetu.

Kwa habari zaidi kumhusu Lameck Ditto unaweza kutembelea tovuti yake kupitia www.lameckditto.com na pia unaweza kumfuata kupitia mtandao wa Twitter @Lameckditto


Read more: LAMECK DITTO: ALIPOTOKA,ALIPO NA ANAPOOTA KUFIKA(INTERVIEW) - BongoCelebrity

No comments:

Post a Comment