|
MWENYEKITI wa Shirika la Ushirikiano wa Tanzania na nchi ya China SINOTA Friendship Association Bw. Jiang Jing Ying leo asubuhi alishindwa kuvumilia na kujikuta akimwaga machozi baada ya kukutana na wastaafu wenzie waliofanyakazi pamoja Reli ya TAZARA miaka zaidi ya 40 iliyopita |
|
Bw. Jing alikutana na wastaafu hao wa TAZARA na kuona hali zao za maisha ambapo mara baada ya kumaliza kusalimiana nao alianza kumwaga machozi akikumbuka namna ambavyo aliishi nao miaka hiyo huku wakiwa katika hali mbaya ya maisha tofauti na jinsi yalivyo maisha yake nchini China. |
|
Alisema kuwa ushirikiano uliodumishwa na marais wastaafu wa Tanzania Hayati Mwalimu Nyerere wa Tanzania na Hayati Mao Tse Tung wa China unapaswa kuendelezwa kwa kudumisha rasilimali zilizoachwa ikiwemo reli ya TAZARA ambayo inapaswa kutunzwa.
|
|
Bw. Ying ambaye pia ni Mkurugenzi wa makampuni kadhaa nchini China anasema kuwa hakutegemea kuwaona watu aliofanya nao kazi wakiwa katika hali duni ya maisha huku wengine wakiwa wamezeeka wakionekana wakishindwa kuendesha maisha yao kutokana na hali ngumu ya uchumi waliyonayo. |
|
Alisema kuwa reli ya TAZARA imechakaa hali ambayo inaweza kusababisha kuibuka kwa ajali jambo ambalo linaweza kugharimu maisha ya watu, hivyo alishauri kuwepo na mikakati mbadala ya kuirejesha reli ya TAZARA katika hadhi yake kama ilivyokuwa miaka ya sabini. |
Bw. Ying anakumbuka alivyofanya kazi kuanzia Kurasini Jijini Dar es salaam kati ya mwaka 1969 na baadaye Kisarawe kisha alihamia Mbeya na Mbozi hadi Tunduma ambako,amepanga kufanya ziara ya kuitembelea reli hiyo kuanzia Tunduma hadi Dar es salaam ambako amepanga kukutana na Rais Jakaya Kikwete ili amweleze mambo muhimu juu ya uboreshaji wa reli TAZARA.
No comments:
Post a Comment