Tuesday, July 24, 2012

MUINGEREZA KUONGEZA NGUVU TIMU YA UTETEZI KESI YA RUFAA YA SAGAHUTU

 

Na Gladness Mushi wa Fullshangwe- Arusha
 
Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imemruhusu mshauri wa masuala ya sheria wa Uingereza, Wayne Jordish kuongeza nguvu katika timu ya utetezi wakati wa kusikiliza rufaa ya afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Kapteni Innocent Sagahutu.
‘’Ushiriki wa Jordish wakati wa kusikiliza rufaa utakuwa na manufaa kwa Sagahutu na utasaidia Mahakama ya Rufaa kuelewa kwa undani hoja za rufaa,’’ Majaji wanaeleza katika uamuzi wao na nakala yake kupatiwa Shirika la Habari la Hirondelle Jumatatu.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, Jordish atazungumza mbele ya mahakama hiyo na kutoa ushauri  kwa timu ya utetezi ya Sagahutu bila kudai malipo yoyote kutoka mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa.
Wajumbe wengine katika timu ya utetezi ya Sagahutu ni pamoja na Wakili Kiongozi, Fabien Segatwa na Msaidizi
wake Scott Martin. Tarehe ya kusikiliza rufaa hiyo bado haijapangwa.
Katika rufaa yake, Sagahutu anapinga hukumu iliyotolewa na mahakama ya awali Mei 17, 2011katika kesi ijulikanayo kama Military II, akishitakiwa katika kesi moja na maafisa wenzake watatu ambao ni pamoja na Majenerali wawili, Augustin Bizimungu na Augustin Ndindiliyimana na Meja Francois-Xavier Nzuwonemeye.
Wote walitiwa hatiani kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. Wakati Bizimungu alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, mwenzake, Ndindiliyimana alihukumiwa adhabu ya muda aliokwishatumikia tangu atiwe mbaroni Januari 29, 2000. Nao Nzuwonemeye na Sagahutu walipewa adhabu ya kutumikia miaka 20 jela kila mmoja wao.
Jordish alishawihi kuwa katika timu za utetezi katika kesi mbili tofauti ICTR ikiwa ni pamoja na ya Meya wa zamani wa Rwanda, Ignace Bagilishema ambaye aliachiwa huru na Michael Bagaragaza ambaye ameshahitimisha kutumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka minane jela.





No comments:

Post a Comment