Saturday, July 28, 2012

YANGA YATWAA KOMBE LA KLABU BINGWA YA SOKA AFRIKA MASHARIKI NA KATI (KOMMBE LA KAGAME)

 



Yanga wakishangilia Kombe lao baada ya kukabidhiwa
Kiiza akishangilia bao la kwanza alilofunga dakika ya 44
Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la kuongoza
Said Bahanuz wa Yanga akimtoka Beki wa Azam,Aggrey Moris.
Mshambuliaji wa Yanga,Hamis Kiiza akiondoka na mpira huku mlinzi wa Azam,Jabir Aziz akimkimbiza kwa kutaka kumzuia mshambuliaji huyo.
Mlinzi wa timu ya Azam,Said Moradi akiwania mpira na Mshambuliaji wa Timu ya Yanga,Said Bahanuz wakati wa mchezo wa fainali ya Mashindano ya Cecafa Kagame cup.
Mashabiki nao hawakua nyuma wakati wa ushangiliaji


YANGA ya Dar es Salaam imetwaa Kombe la Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0.

Yanga sasa imebakiza mara moja kufikisha idadi sawa na wapinzani wao wa jadi, Simba kutwaa Kombe hilo, mara tano kwa sita. Yanga ilibeba taji hilo 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012.

Mashujaa wa Yanga leo walikuwa Hamisi Kiiza aliyefunga bao la kwanza dakika ya 44 na Said Bahanuzi aliyefunga la pili dakika ya tatu ya muda nyongeza, baada ya kutimu dakika 90 za mechi hiyo.

Kiiza alifunga bao lake, baada ya kuuwahi mpira uliookolewa na kipa Deo Munishi ‘Dida’ na kumpiga chenga kipa huyo kisha kuusukuma mpira nyavuni.

Bahanuzi aliuwahi mpira mrefu uliopigwa na beki Oscar Joshua na kuwazidi ujanja mabeki wa Azam kabla ya kumtungua Dida.

Mechi hiyo imechezeshwa vema na refa Thierry Nkurunzinza kutoka Burundi, akisaidiwa na Simba Honore wa Rwanda na Peter Sabatia wa Kenya, wakati mezani atakaa Issa Kagabo wa Rwanda, Kamisaa Hassan Amir wa Somalia na Mtathmini wa marefa ni Anangwe Robert wa Kenya.

Katika mchezo uliotangulia wa kusaka mshindi wa tatu, AS ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliifunga APR ya Rwanda mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na Magola Mapanda dakika ya 18 na Mutombo Kazadi dakika ya 67, wakati la kufutia machozi la timu ya jeshi la Rwanda, lilifungwa na Jean Mugiraneza dakika ya 89.

No comments:

Post a Comment