Friday, September 14, 2012

Harusi ya Tsvangirai yasitishwa



Tsvangirai na mpenzi wake
Mahakama nchini Zimbabwe imesitisha harusi ya Waziri Mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai iliyotarajiwa kufanyika hapo kesho kama ilivyokuwa imepangwa.
Mahakama imesema kuwa Tsvangirai tayari ana mke.
Mapema wiki hii mahakama kuu nchini humo ilitupilia mbali madai ya Locadia Tembo aliyesema kuwa yeye ni mke wa kitamaduni wa Bwana Tsvangirai na kusema kuwa ndoa za kitamaduni hazitambuliki kisheria.

Lakini sasa Hakimu amekubaliana na Locadia na kuamuru harusi iliyopangwa kufanyika siku ya Jumamosi haitafanyika tena.
Hii ni licha ya baadhi ya viongozi wa nchi mbali mbali walioalikwa kwa harusi kuwasili nchini humo.
Mawakili wa Tsvangirai wanataka mahakama kutoa amri ya dharura na kuruhusu harusi hiyo kuendelea kama ilivyopangwa.
Kesi nyingine ambayo mahakama ilisikiza leo dhidi ya Tsvangirai ni ya mwanamke mmoja kwa jina Nozipho Shilubane aliyesema kuwa Waziri Mkuu huyo aliahidi kumuoa.
Baadhi ya wadadisi wanasema kuwa kesi hiyo ni dalili ya njama za kisiasa kumpaka tope waziri mkuu kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka ujao. Tsvangirai atatoana jasho na rais Robert Mugabe katika uchaguzi huo.
Lakini wengine wanasema kuwa Tsvangirai hana wa kulaumu ila yeye mwenyewe kwani amejihusisha na wanawake wengi baada ya mke wake kufariki katika ajali ya barabarani mwaka 2009 baada ya waziri mkuu kuchukua wadhifa wake.
Mwandishi wa BBC Brian Hungwe mjini, Harare, anasema kuwa harusi hiyo ilipangwa kufanyika katika mtaa mmoja wa kifahari mjini Harare.
Rais Mugabe anatarajiwa kuandaa dhifa maalum kwa viongozi wa nchi za kiafrika walioalikwa kuhudhuria.

No comments:

Post a Comment