Sunday, September 9, 2012

MAPENZI MOTOMOTO;KUSHIKWA KWENYE MAPENZI SIYO LIMBWATA AU MAPENZI MOTOMOTO BALI NI MATOKEO YA HOMONI!


Wakati mwingine huwapigia simu wapenzi wao wa nje waziwazi

Tunajiuliza siku zote ni kwa nini penzi linapoingia mahali huweza kuharibu kila kitu? Tumekuwa na misemo yetu ya siku nyingi kama siyo ya asili, kama vile ule wa ‘penzi ni ulevi’ au ‘penzi ni upofu’ na mingine yenye kuonyesha kwamba penzi lisipoangaliwa kwa makini linaweza kuleta athari mbaya na kubwa kwa binadamu.

Ni nani ameshawahi kujiuliza ni kwa nini hali hiyo hutokea? Kuna yeyote ambaye hata mara moja ameshawahi kujiuliza ni kwa nini penzi halina shujaa au mnyonge pale linapoingia wote huwa kama waliopagawa? Bila shaka sio wengi, kama wapo ambao wameshawahi kujiuliza swali hili. Kila mmoja anadhani ndivyo ilivyo na hakuna awezaye kujua ni kwa nini.

Ukweli ni kwamba penzi halina tofauti na ulevi sugu kama ule wa pombe au madawa ya kulevya. Penzi linaelezwa kwamba ni sawa na ubobeaji wa mcheza kamari. Ile starehe na pumbazo la akili ambalo mtumiaji wa madawa ya kulevya au mlevi sugu analihisi, ndilo hilo hilo ambalo mtu aliye katika mapenzi anahisi.

Penzi(Kwa maana ya mtu kumpenda mwingine wa jinsia tofauti kwa penzi la kawaida au hadi kwa kufanya mapenzi) na usugu wa madawa au pombe, vyote huwa vinauchochea mwili wa anayehusika kutoa homoni inayofahamika kama dopamine. Homoni hii ambayo ni kemikali katika ubongo huwa inaujaza mwili raha na ni kemikali hii hii ndiyo ambayo inahusika katika kuupa mwili tabia ya usugu katika mambo fulani kama ulevi.

Ni kitu gani kikubwa katika hili?

Ni kwamba kama ni hivyo, ina maana kuwa mtu kuwa kwenye kiwango kikubwa au cha juu cha kupenda, yaani kama tulivyozea kusema ‘kuwa hoi kwa penzi’, ni sawa na wakati ule mlevi sugu wa madawa akiwa ameshavuta au kunywa.

Mbaya zaidi ni pale penzi linapofikia hatua ya kuwa penzi la kukutana kimwili. Ni mbaya kwa sababu katika hatua hii homoni ya depomine inayotolewa inaweza kuizinga akili milele.

Kinachotokea ni kwamba kama homoni hiyo itajizinga kwenye akili, mhusika anakuwa sawa kabisa na mlevi sugu wa pombe au madawa ya kulevya, inakuwa ni vigumu sana kumtoa mtu kama huyo kwenye penzi na huyo fulani wake.

Bila shaka umeshawahi kuona au kusikia juu ya watu ambao wanaishi kwenye uhusiano mgumu sana na wapenzi wao, lakini bado wakawa wagumu wa kuondoka kwenye uhusiano huo. Kwa mawazo yetu wengi huwa tunadhani kung’ang’ania huku kunatokana na hali kama utegemezi, hasa kwa wanawake.

Baadhi yetu huwa tunaamini kwamba hali hiyo inaweza kuwa inasababishwa na dawa za asili au uchawi maarufu kama Limbwata, hasa pale mwanaume anapokuwa ameshikwa kwenye mapenzi na mpenzi wake au mkewe. Hii sio kweli.

Kuna wakati unakuta kwamba mwanamke ana uwezo wa kuendesha maisha yake na pengine yeye ndiye anayemsaidia mwanaume katika maisha, lakini pamoja na kuteswa au kuburuzwa na mwanaume huyo, bado atang’ang’ania kuishi naye. Kuna wakati tunaona kabisa kwamba, mwanaume anajua kwamba mwanamke anamfurusha kwenye uhusiano wao na anakiri, lakini bado anang’ang’ania kwenye uhusano huo na mwanamke huyo.

Inaanzaje?

Watu wawili hupendana. Kama nilivyosema, kupendana huku husababisha homoni hii kuzalishwa ubongoni. Kuzalishwa kwa kemikali hii ndiko ambako humfanya mtu aliyependa kuwa katika raha fulani isiyoelezeka. Kama ilivyo kwa mlevi wa pombe au madawa ya kulevya, kuna wakati kiwango cha nishai hushuka ambapo inabidi avute au kunywa tena. Kwa mtu aliyependa naye, kuna wakati hali ya raha hii hushuka, kutegemea mazingira.

Lakini kama wapendanao wamekutana kimwili na kukutana huko kukawapa raha kubwa sana, uwezekano wa kemikali hii kuizinga akili moja kwa moja ni mkubwa sana. Akili inapozingwa na homoni hii, mpendaji kamwe hataacha tena kumpenda huyo mtu wake.

Inakuwa kama mlevi sugu anavyotegemea pombe au madawa kupata raha ya maisha, huyu mpendaji naye atakuwa hajisikii raha bila kuwa na huyo mpenziwe, bila kujali visa na vibweka anavyomfanyia. Hata kama hashiriki naye tendo la ndoa, bado atakuwa anajisikia raha tu kuwa naye.

Msomi mmoja wa chuo kikuu cha Guelph huko Canada, George Bubenik anakiri kuwepo kwa hali hii na anasema ndio maana unaweza kukuta mtu akiishi kwenye ndoa ya mashaka na vurugu huku huku wengine wakishangaa na kutoelewa sababu. “Mtu ambaye anafurahia sana tendo la ndoa mwanzoni mwa uhusiano na mwenzake anaweza kung’ang’ania kwenye ndoa hata kama imejaa vurugu”

Anasema watu hawa wangetarajiwa kuondoka au kuzikimbia ndoa za aina hii lakini huwa hawafanyi hivyo kwa sababu wamepata usugu wa kiakili kwa zile hisia wanazozipata wakati waliposhiriki tendo la ndoa na wapenzi wao. Kama mlevi sugu wa pombe asivyoweza kuacha pombe hata kama inakaribia kumuuwa, ndivyo inavyokuwa kwa watu wa aina hii.

Haina maana kwamba hao wapenzi wao ni watu wenye kujua sana mapenzi, hapana. Ni kwamba siku ya kwanza walipokutana , ubongo ulizalisha homoni kwa wingi na ikawa imeizinga akili. Kinachojirudia hapa ni zile hisia za awali. Sawa kabisa na mlevi sugu, ambaye anaweza kuwa anakunywa pombe kali na isiyo na utamu, kwa sababu anachohitaji siyo ladha ya pombe, bali zile hisia wakati au baada ya kunywa. Hapa mwanamke au mwanaume aliye katika hilo penzi anaendeshwa na hisia anazozipata wakati wa tendo la ndoa, ambazo zimeganda akilini kupitia homoni hii ya dopamine.

Huwa hakuna kulogwa wala limbwata au mapenzi motomoto, hapana., hapa kuna tatizo la utegemezi. Mhusika ni mtu ambaye inabidi asaidiwe kama anavyosaidiwa mlevi sugu. Wengi wetu huwalaumu watu hawa au wapenzi wao, jambo ambalo bila shaka siyo haki.

Tumeshawahi kusikia bila shaka watu wakisema, ‘wewe hujui ni kwa nini anang’ang’ania uhusiano ule, anajua mwenyewe anachokipata’. Wengi wanaposema hivyo wana maana ya kile mtu huyo king’ang’anizi anachokipata hadi kutokuwa tayari kuvunja uhusiano na mpenzi anayemtesa au kumdhalilisha. Mara nyingi wana maana ya mapenzi motomoto ya kitandani. Huu siyo ukweli hata kidogo, kwani unaweza kukuta hata mapenzi ya kitandani mtu huyo hapati. Anachokipata hapa ni ridhiko linalotokana na dopamine iliyozinga ubongoni mwake.

Inakuwaje ikibidi uhusiano huo ufe:

Kuna wakati kwa sababu ya mazingira fulani fulani inabidi uhusiano huu ufe, hata kama mmoja ni king’ang’anizi vipi. Hilo linapotokea yule king’ang’anizi hukabiliwa na athari za matokeo kama vile wasiwasi, aina ya hamu ya mapenzi au kupendwa isiyoweza kuridhishwa, huzuni na hasira. Hali hizi pia huwa zinapatikana kwa mlevi au mvutaji sugu ambaye anajaribu kuacha kuvuta au kunywa.

Kuthibitisha hii Bubenik aliwafanyia utafiti panya wadogo wa porini na kugundua kwamba wanyama hawa wakizuiwa wasitoe homoni iktwayo oxytocin ( sawa na homoni ya dopamine kwa binadamu) wakati wakipandana huwa hawadumu pamoja. Lakini pale wanapoachiwa watoe hiyo homoni huwa hawaachani hadi kufa.

Tunaweza kusema mtu kushikwa au kunaswa kwenye mapenzi ni suala ambalo hakuna mtu anayeweza kudai kwamba anaweza kulizuia. Kulizuia kunawezekana kama mtu ataamua kuachana na tabia ya uzinzi tu, kwani hatafikia mahali ambapo akili yake itazingwa na homoni hii.