Wednesday, September 5, 2012

MWILI WA KARDINALI LAUREAN RUGAMBWA KUZIKWA UPYA OKTOBA 6, BUKOBA


 
Marehemu Kardinal Laurean Rugambwa enzi ya uhai wake. 
Kanisa kuu katoliki jimbo la Bukoba ambalo masalia ya marehemu kardinali Rugambwa yatazikwa ndani yake.
Kanisa katoliki nchini dayosisi ya Bukoba mkoani Kagera, wanajiandaa kuzika upya masalia ya mwili wa aliyekuwa askofu wa dayosisi hiyo Kardinali Laurean Rugambwa, aliyefariki mnamo mwaka 1997 katika kanisa kuu la Bukoba. Maziko ya Kadinali Rugambwa yamepangwa kufanyika siku ya oktoba 6 mwaka huu.
Mwili wa askofu huyo wa kwanza nchini na Kardinali wa kwanza mweusi barani Afrika umezikwa katika kanisa la kwanza mkoani Kagera lililopo Kashozi kutokana na kwamba kanisa kuu la Bukoba ambalo marehemu aliagiza kuzikiwa ndani yake lilikuwa katika matengenezo makubwa.
Akizungumza katika kipindi cha Baragumu Channel ten na baadaye kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Askofu msaidizi wa Jimbo la Bukoba Askofu  Methodius Kilaini , amesema wanataka kumzika kardinali Rugambwa kwa heshima tena katika kanisa alilopenda kuzikiwa kutokana na kukamilika kwake, lakini kabla ya kuzikwa humo kutatanguliwa na ibada mbalimbali ikiwa sehemu alikozaliwa, alikobatizwa, sherehe zitakazoambatana na kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwa kardinali Rugambwa tarehe 7 mwezi Octoba.
“tuna alika watu wengi kuhudhuria kwenye tukio hili…, na pia tunakaribisha michango itakayowezesha kuwa na kitu cha kumkumbuka marehemu kwa mchango wake…. alisema askofu Kilaini.

Naye mmoja wa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya kufanikisha tukio hilo , James Rugemalira, alimwelezea Kardinali Rugambwa kama mtu aliyetoa mchango mkubwa kwenye jamii ya watanzania, kuanzia kwenye nyanja za elimu, afya na kiroho.

Marehemu Kardinali Rugambwa ana mambo mengi ya kukumbukwa na jamii ya watanzania hususani watu wa mkoa wa Kagera hasa kwa juhudi zake za kupeleka elimu mkoani humo kwa kuagiza ujengwaji wa shule za msingi na sekondari ikiwemo shule ya kwanza ya wasichana ya Rugambwa ambayo ujenzi wake ulikuwa ni mafanikio ya marehemu huyo kuomba msaada wa ujenzi wa shule hiyo alipohutubia bunge la Ujerumani akiwa mwafrika wa kwanza.Licha ya mambo hayo yote kanisa hilo pia liko mbioni kuanzisha mfuko rasmi wa kumuenzi kardinali huyo mfuko utakaojulikana kwa jina la Kardinali Rugambwa ambao utakuwa maalumu kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

Padre Laurean Rugambwa aliwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 10 Februari,1952.Alizaliwa julai 22 1912 na kufariki miaka 15 iliyopita.