Tuesday, September 18, 2012

Obama na rafiki yake wa Uganda


Kijana Christopher Kule na babake Dasiel Raul


Kama kuna rais ambaye watu wengi Uganda wangetaka kukutana naye ni rais wa Marekani Barack Obama.
Kijana Christopher Kule, mwenye umri wa miaka kumi na ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi wilayani Kasese, nchini Uganda, hajaachwa nyuma katika ndoto hiyo.
Kijana huyo anaamini kuwa baada ya kuandikiana barua na Rais Obama, kuna matumaini kwamba siku moja atakutana naye.
Yote haya yanatokana na zoezi la kuandika barua ambalo Kule na wanafunzi wenzake walikuwa wanafanya darasani, baada ya kuagizwa na mwalimu wamwandikie barua mtu yeyote wakiomba msaada kwa jamii yao.
Barua ya Kule bila shaka ilimtia hamasa mwalimu wake wa kigeni kutoka Marekani ambaye alikuwa anafunza shuleni humo kwa muda.
Mwalimu huyo alisema kuwa nyanyake ni rafiki wa mmoja wa wasaidizi katika ikulu ya rais na kuahidi kuhakikisha kuwa ujumbe huo utamfikia rais Obama na bila shaka ahadi ikatimizwa , kwani barua ilimfikia rais Obama.
Kule alisema kuwa katika barua yake, alimwomba Obama kusaidia Uganda kuangamiza uasi na kuhamasisha amani.
Katika majibu yake kwa Kule, rais Obama alisema kuwa Marekani imejitolea kuangazia maswala kadhaa muhimu kote duniani kama haki za binadamu kwa sababu Marekani inapinga vikali ghasia na ukandamizaji dhidi ya watu wote. Pia alimtumia kijana huyo picha yake aliyokuwa ametia saini.
Rais Obama alipata muda wa kumjibu kijana Kule. Je marais wa Afrika wana muda wa kuzungumza na wananchi wao na kutoa mfano wa Obama kwa Afrika? Nini maoni yako? Sema nasi katika ukurasa wetu wa Facebook bbcswahili.