Friday, December 7, 2012

NYOTA WA SIMBA, YANGA WAZIUA KILI STARS, Z'BAR HEROES.... FAINALI CHALENJI NI UGANDA v KENYA


Kiungo wa Kilimanjaro Stars, Mwinyi Kazimoto (kushoto) akichezewa madhambi na Godfrey Walusimbi wa Uganda 'The Cranes' wakati wa mechi yao ya nusu fainali ya michuano ya Cecafa Challenge Cup kwenye Uwanja wa Nelson Mandela leo jioni. Uganda ilishinda 3-0.

Wachezaji wa Zanzibar Heroes wakiwania mpira dhidi ya wachezaji wa Kenya wakati wa mechi yao ya nusu fainali ya michuano ya Cecafa Challenge Cup kwenye Uwanja wa Nelson Mandela leo jioni. Uganda walishinda kwa penalti 4-2 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 2-2.

MABINGWA mara 12 wa Kombe la Chalenji la nchi za Afrika Mashariki na Kati, Uganda na mahasimu wao Kenya watacheza mechi ya fainali keshokutwa Jumamosi baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole leo. 

Wenyeji Uganda waliwafunga Tanzania Bara kwa magoli 3-0, katika mechi iliyochezwa kuanzia saa 1:00 usiku, ambayo ilitanguliwa na ya nusu fainali ya kwanza ambayo iliwashuhudia Zanzibar wakipoteza uongozi mara mbili katika sare ya 2-2 ndani ya dakika 120 kabla ya kulala kwa 'matuta' 4-2. 

Uganda waliizidi Tanzania Bara kwa kila kitu katika ushindi uliostahili wa 3-0, ulioendeleza rekodi safi ya wenyeji ya kushinda mechi zote za Chalenji kufikia sasa mwaka huu huku wakiwa hawajaruhusu hata goli moja langoni mwao. 

Ushindi kwa wenyeji unamaanisha kwamba watacheza fainali keshokutwa saa 1:00 usiku dhidi ya Kenya, ambao pia waliwafungia 1-0 katika mechi ya ufunguzi wa Kundi A, huku Tanzania Bara na Zanzibar zikiuweka undugu kando katika katika kuwania nafasi ya tatu mapema saa 10:00 jioni keshokutwa pia. 

Uganda, ambao hawajafungwa mechi yoyote kwenye ardhi yao katika michuano yote tangu mwaka 2004 -- wakizikalisha hata timu kubwa kama Nigeria, Angola na Zambia -- waliwanyanyasa Watanzania uwanjani hadi majukwaani ambako baadhi ya mabango ya mashabiki yalisomeka: "Hata Hispania hainusuriki Namboole", "Rest In Peace Tanzania" na "Why Always Uganda?" 

Nyota wa wanaochezea klabu za Simba na Yanga na wengine waliopata kuchezea klabu hizo miaka ya nyuma ndiyo walioongoza mauaji kwa timu zotembili za Tanzania.

Mshambuliaji anayechezea klabu ya Simba, Emmanuel Okwi aliifungia Uganda goli la kuongoza katika ya dakika ya 11 kwa shuti kali lililogonga 'besela' la lango la kipa wa klabu yake ya Simba, Juma Kaseja, na kutinga wavuni baada ya kuiwahi vizuri pasi ya kupenyezewa kutokea upande wa kulia. 

Uganda ilipata goli la pili katika dakika ya 51 kupitia kwa nyota wa zamani wa Simba pia, Robert Ssentongo, aliyefunga kutokea jirani na lango kufuatia krosi ya mshambuliaji wa klabu ya Yanga, Hamis Kiiza, aliyeingia kuchukua nafasi ya Okwi ambaye aliumia katika dakika ya 36.

Makosa ya kipa Kaseja ya kutema mpira wa 'fri-kiki' iliyopigwa na Joseph Ochoya, yaliizawadia Uganda goli la tatu lililofungwa na Ssentongo tena.

Kenya ilimstaafisha kocha wa Zanzibar, Salum Bausi, ambaye alishaahidi mapema kabla ya kuanza kwa michuano hiyo kwamba ataachia ngazi iwapo atashindwa kurejea mafanikio yao ya mwaka 1995 ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo. 

Bausi alisema baada ya kipigo hicho kwamba amejiuzulu rasmi na kwamba anawaachia nafasi hiyo watu wengine. 

Zanzibar ilipoteza uongozi mara mbili na kuwaruhusu Kenya kusawazisha kutokana na makosa ya ulinzi.

Wakati Zanzibar wakiongoza kwa goli 1-0 lililofungwa na Khamis Mcha, beki wa kati na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' alijifunga kwa kichwa wakati akijaribu kuokoa shuti la juu.

Zanzibar walipata goli la pili kwa penalti iliyofungwa na beki, Aggrey Morris katika kipindi cha pili lakini makosa ya kipa Mwadini Ali aliyeshindwa kuucheza mpira wa kona na yalimpa fursa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mike Baraza kufunga kirahisi kwa kichwa.

Tanzania Bara na Zanzibar watawania zawadi ya mshindi wa tatu ambayo ni dola 10,000. Bingwa ataondoka na kombe na dola 30,000 wakati washindi wa pili watapata dola 20,000.

Timu zilikuwa; Uganda: Hamza Muwonge, Dennis Iguma, Godfrey Walusimbi, Isaac Isinde, Henry Kalungi, Godfrey Kizito, Moses Oloya, Hassan Waswa, Robert Ssentongo, Said Kyeyune na Emmanuel Okwi/ Hamis Kiiza (dk.36). 

Tanzania Bara: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Amri Kiemba, Salum Aboubakar 'Sure Boy'/ Athumani Idd 'Chuji', Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa na John Bocco.

No comments:

Post a Comment