Na Mussa Juma, Arusha -JUMLA ya wanafunzi 6,838 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu, mkoani Arusha, wamekosa nafasi ya kujiunga na masomo ya Sekondari kutokana na uhaba wa nyumba vya madarasa 172 .
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Evelyine Itanisa alitoa taarifa hiyo, juzi katika kikao cha kamati ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 mkoani Arusha.
Itanisa alisema wanafunzi hao, wanatoka katika halmashauri sita za mkoa Arusha na ni halmashauri moja tu ya Karatu ambayo imeweza kuwachukua wanafunzi wote waliofaulu mwaka huu.
Alisema katika jiji la Arusha wanafunzi 2420 wamekosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa 61, Ngorongoro wanafunzi 441 wamekosa nafasi kutokana na uhaba wa vyumba 11.
Alisema Halmashauri ya Arusha vijijini wanafunzi 1880 wameshindwa kujiunga na sekondari kutokana na uhaba wa vyumba 47.
“Pia Halmashauri ya Longido kuna wanafunzi 140 ambao wanahitaji madarasa manne, Meru wanafunzi 1,159 wakiwa na mahitaji ya vyumba 29, wilaya ya Monduli wanafunzi 807 wamekosa nafasi kutokana na kukosekana madarasa 20”alisema Itanisa.
Alisema kutokana na hali hiyo, ameziagiza halmashauri hizo sita za mkoa wa Arusha kuiga mfano wa halmashauri ya Karatu, kwa kuhakikisha zinajenga vyumba vya madarasa vya kutosha ili kuhakikisha wanafuzi wote waliofaulu wanapata nafasi.
“Ili kuhakikisha watoto waliofaulu wote wanaendelea na sekondari, kila halmashauri inapaswa ihakikishe inakamilisha ujenzi wa madarasa kabla ya februari mwakani “alisema Itanisa.
Hata hivyo, Katibu Tawala huyo alisema kiwango cha ufaulu kwa Mkoa wa Arusha, kimekuwa kikipanda kwa miaka mitatu sasa mfululizo ambapo mwaka huu jumla ya wanafunzi 26,464 wamefaulu mitihani kati ya wanafunzi 37,493 waliofanya mitihani.
“Matokeo haya yanafanya Mkoa wa Arusha uwe umefaulisha kwa asilimia 70.6 na waliofaulu ni wavulana 12,608 na wasichana 13,856”alisema Itanisa.
No comments:
Post a Comment