Wednesday, February 6, 2013

Kuondokewa hoja binafsi bungeni ni kuwasaliti wananchi

Na Bryceson Mathias
TABIA ya kujadiliwa kwa hoja za Mawaziri wa Elimu, Mafunzo na Ufundi Shukuru Kawambwa, na wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na hatimae kuungwa mkono na Wabunge wa Vyama vyao, zimetafsiliwa kama ni Kuwasaliti wananchi waliowapa Kura.
Sababu ya kutafsilika hivyo, kumetokana na kwamba mara zote zimekuwa zikipendekeza kuondolewa bungeni kwa hoja binafsi zilizowasilishwa mapema na wabunge wa upinzani, ambazo wananchi wanaona zina dhima ya Mustakabali wa Taifa.
Hoja binafsi zilizohasimiwa na mawaziri hao ziondolewe ni pamoja na Udhaifu wa Sekta ya Elimu iliyowasilishwa na Mbunge wa kuteuliwa James Mbatia-NCCR Mageuzi, na ya Maji ambayo mapema iliwasilishwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Kinachopelekea tafsiri hizo, ni pamoja na Mawazi wa Wizara zingine kutoweka pingamizi la kuondolewa kwa Hoja binafsi ya Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba kuhusu mikopo ya Elimu ya Juu.
Hoja nyingine ni ile ya Mbunge wa Nzega Dk. Hamisi Kigwangala ya mpango maalumu wa kukuza ajira kwa vijana kwa kuanzisha mfuko wa mikopo 
ya vijana wanaowekeza kwenye kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja 
kwa moja na kilimo kwa hoja Mbadala za
Kama ilivyofanyika kwa Mbatia alipowasilisha Hoja ya Udhaifu wa Sekta ya Elimu, ndivyo ilivyofanyika kwa Mnyika katika hoja yake aliyokuwa akitaka Bunge liazimie kuitaka Serikali ichukue hatua za haraka ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la Dar es Salaam.
Hapa ndipo nilipoona umuhimu wa wa bunge hili la kichama na kishabiki kuwa ni kubadilisha utaratibu katika katiba mpya, spika na naibu wake wasiwe wabunge na wasiwe na chama chochote cha siasa, na mawaziri nao wasiwe wabunge.
Sikubaliani kwamba kila kinachoongelewa na upinzani ni cha kubeza, ieleweke kuwa, ukiyakataa mapendekezo ya upinzani si kana kwamba umewapinga wao bali unakuwa umewapinga wananchi walioko nyuma yao.
Kilicho mbele yetu, tunatakiwa tuweke Utaifa kwanza na kasha ndipo vyama vyenu baadae. Lakini nimehuzunishwa sana na mwenendo wa Bunge letu, ambalo sasa naona limekuwa halina utaifa kwa baadhi ya wabunge, bali limegubikwa na uvyama.
Wananchi sasa tunaamini kwamba, kila inapotolewa hoja ya manufaa kwa wananchi hasa inapotolewa na wapinzani, Spika au Naibu Spika wa Bunge anaizima, hivyo kwa tabia na muktadha huo, tunajua wabunge wa chama cha cha mapinduzi (CCM), wameamua kututesa wananchi , Je. Hawajui mwaka 2015 uko mlangoni?.
Kiukweli mpaka sasa, Bunge limewaonesha wananchi kwamba halina maadili, na lawama zote lazima tuwatupie wasimamizi wa Bunge wakiongozwa na Spika na Naibu Spika. Lazima ifike mahali wabunge waogope na kuona jinsi wapiga kura walivyopigwa Jua na Mvua ili kuwafanya wawe wawakilishi wao, kuliko hivi wanavyoisimamia Serikali kinafiki.
Hivi wabunge; Je,mmesahau kabisa kwamba kuna watu wanakufa huku na nchi iko katika hali mbaya kwa njaa,,, migogoro ya kijamii na kidini, elimu haina mwelekeo wala haimuandai mtanzania kujitegemea zaidi ya kuwa mtumwa wa ajira
Aidha najihoji moyoni Je, baadhi yenu mtapataje uchungu kama mishahara yenu imefikia million tatu nukta sita ukiondoa marupurupu!! Basi kama tatizo ni siasa,,,Rais Kikwete licha ya juhudi zake zinazosemekana ni nyingi ili atakapokabidhi kijiti aweze kukumbukwa, Wabunge hawa ndio watu uliopewa na wananchi ili wakusaidie kutokomeza Umasikini, Ujinga na Maradhi.