Tuesday, February 12, 2013

Spika Anne Makinda apokea sms 600 zenye wito wa kumtaka kujiuzulu na matusi

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anne Makinda.

Inaripotiwa kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, amepokea jumbe za maneno 400 na za miito ya simu 200 zenye matusi ya nguoni kutoka kwa watu wakimtaka ajiuzulu. Mtoa habari wa HabariLeo ambaye yupo karibu na Spika Makinda amesemea jumbe hizo zimerekodiwa.Kwamba, Spika alianza kupokea jumbe hizo kuanzia juzi, baada ya viongozi wa CHADEMA kutangaza namba za simu za Spika kwenye mkutano wa hadhara na kuendelea jana ili kutumia ‘nguvu ya umma’, kumlazimisha ajiuzulu. 



Sababu ya kutumwa jumbe hizo inaripotiwa kuwa ni baada ya hatua ya Spika Makinda kutangaza mabadiliko ya Kamati za Bunge, yaliyoivunja Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na shughuli zake kuwekwa chini ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambapo katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Mwenyekiti wa POAC, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe hakuridhishwa nayo na hivyo kumshitaki Spika Makinda kwa Wananchi ili wamng’oe.


Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah, alipozungumza na gazeti hili juzi, alisema uamuzi huo haukufanywa na Spika Makinda peke yake, bali ni baada ya kushauriana na Kamati ya Kanuni za Bunge, ambayo iliridhika na sababu za kuchukuliwa uamuzi huo.
Wajumbe wa Kamati iliyoridhia makubaliano hayo mbali na Spika na Naibu Spika, ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA). Wengine ni Mbunge wa Mbulu, Mustapha Akunaay (CHADEMA), Mbunge wa Kibondo, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF). Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM), Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM) na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM).
Dk Kashilillah alisema mabadiliko hayo hayakuigusa kamati ya POAC peke yake, bali kamati zingine kama ya Sheria Ndogo na ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, ambayo imegawanywa mara mbili.
Akielezea sababu za kuvunja POAC, Dk Kashilillah alisema lengo lilikuwa ni kuunganisha wizara, taasisi zake na mashirika yaliyo chini ya wizara husika, ili yawe na msemaji mmoja. 
Alisema awali Waziri alikuwa anawajibika PAC, wakati mashirika ya umma yaliyo chini ya wizara yakiwajibika chini ya POAC.
Kwa mujibu wa Dk Kashilillah, kulikuwa na mkanganyiko mkubwa na akaeleza kuwa hatua ya kuunganisha wizara na mashirika yake ya umma, kutafanya sasa Waziri, Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi na watendaji wakuu wa mashirika, kuwajibika kwa kamati moja ya PAC.
Dk Kashilillah alisema sababu nyingine ni kuangalia utendaji katika baadhi ya nchi, ambazo alisisitiza kuwa hazina kamati za mashirika ya umma.
Mwandishi aliwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambayo iliweka wazi kuwa hakuna sheria yoyote inayozuia mtu kutoa namba ya simu ya mwingine kwa mtu au watu wengine, bila ridhaa ya mwenye namba ya simu.
Ofisa wa TCRA, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu si msemaji wa taasisi hiyo, alisema sheria ya kuzuia utoaji namba na taarifa za mtu mwingine, inakataza kampuni za simu kufanya hivyo, lakini haizungumzi kwa mtu binafsi. Ofisa huyo alinukuu sheria hiyo:

Taarifa ni siri ya mtu husika, isipokuwa kama mtu huyo ameitoa kwa ridhaa yake.

Alisema pamoja na kuwapo na kipengele hicho, mtu yeyote ambaye ana namba ya simu ya mtu mwingine, hazuiwi kutoa namba hiyo kwa watu wengine.Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, wamesema ingawa namba za simu za viongozi hao zinaweza zikapatikana kwa kila mtu, kuzigawa katika mkutano huo ambao ulikuwa na mtazamo hasi kwa Spika na Naibu wake, kulikuwa na nia mbaya.



Kama ungekuwa mkutano au semina yenye nia njema na Spika, ungesema wamegawa simu kwa nia njema. Lakini mkutano huo ulivyokuwa na kauli mbovu kwa Spika na taasisi ya Bunge, kitendo cha kuwapa watu namba kinamaanisha walitaka hao watu wamtukane pia.
katika mkutano kama huo, kunakuwa na watu wa kila aina wakiwamo wasio na busara. Hivyo viongozi hao wa CHADEMA waliofanya hivyo, wameshindwa kutumia busara.
Mjumbe wa NEC, Juma Killimbah, ambaye aliwahi kuwa Mbunge na kuhadharisha wananchi wasije kujikuta katika mkono wa sheria kwa kutumia namba hizo vibaya kwa kutoa matusi, alisema simu ya kiongozi huyo kujulikana si ajabu na ni jambo la kawaida.

Tatizo ni maudhui. Kama kitendo hicho kina lengo zuri hakuna tatizo.

Sehemu ya taarifa hii imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la HabariLeo. via Wavuti.

No comments:

Post a Comment