HISTORIA MKOA KAGERA – KUITWA KAGERA Mkoa huu haukuitwa Kagera bali ulikuwa moja ya maeneo yaliounda jimbo lililoitwa Lake Province. Jimbo hili lilijumuisha Wilaya ya Bukoba, Musoma, Shinyanga na Tabora. Baadaye ulibadilishwa jina na kuitwa ‘West Lake Region’ (Ziwa Magharibi) na kujumuisha Wilaya 4 za Ngara, Biharamuro, Karagwe na Bukoba. Kabla na baada ya kuja kwa wakoloni mkoa wa Kagera ulikuwa na utawala wa Kimila (Chiefdoms) uliogawanyika katika himaya 8. Himaya hizo ni pamoja na Kyamutwara, Kihanja (Kanazi), Kiziba, Ihangiro, Bugabo, Karagwe, Biharamulo (Rusubi) na Maruku (Bukara). Baadhi ya Watemi waliotawala himaya hizo ni pamoja na Emmanuel Rukamba (Kyamtwara), Rumanyika (Karagwe), Kasusura (Biharamulo), Lugomola (Bukara), Rutinwa (Kiziba), Kayoza (Bugabo), Kahigi (Kihanja) na Nyarubamba (Ihangiro). Kila mtemi alikuwa na walinzi wake walioitwa Warugaruga.Wakazi wa asili ya Kagera ni wabantu na wengi wao wana asili ya Bunyoro. Wanaongea lugha sawa na ile ya Wanyoro, Wanyankole, Watoro na Wakiga. Busubi na Bugufi wana lugha na desturi sawa na Watusi, Wahutu na Waha. Lakini makabila hayo ni ya Wabantu wa Ziwa (Interlacustrine Bantu) na yanafanana mila na desturi. Makundi hayo yaligawanyika kati ya wachungaji (Bahima) ambao walitawala na wakulima (Bairu) ambao walitawaliwa na mara nyingi kudharauliwa. Bahima (Balangira) walikuwa na koo chache zipatazo 20 na walitawaliwa na Wahinda, Wabito na Wankango. Bairu walikuwa na Koo kama 130 zenye mashina 24 ambayo kiasili walikuwa Bairu lakini kwa kuoa katika Bahima au kufanya kazi kwa Watemi walipandishwa hadhi na kuwa Bahima (Batware). Kila ukoo uliitwa jina la Baba mwanzilishi wake na kina ukoo ulikuwa na kitu walichokatazwa kula (Omuziro) na mnyama walioshirikishwa nae (Ekyerumono).Mkoa ulibadilishwa jina na kuitwa Kagera mwaka 1979 baada ya vita ya Tanzania na Uganda. Chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo wakati huo Capt. Peter Kafanabo jina la Kagera lilipendekezwa kwa sababu ya mto Kagera unaogusa sehemu kubwa ya Wilaya zote zinazounda Mkoa wa Kagera.
No comments:
Post a Comment