Thursday, August 1, 2013

SHEIKH PONDA ISSA PONDA APENDEKEZWA KUGOMBEA URAIS MWAKA 2015

Ikiwa imebakia miaka miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge hapa nchini,baadhi ya waumini wa kiislamu wameanza kupendekeza wagombea wa urais wanaoona kuwa wanafaa ambapo jina la Sheikh Ponda Issa Ponda limeongoza....

Mapendekezo hayo yamedhihirika katika mihadhara kadhaa anayoifanya Ponda katika mikoa mbalimbali nchini,ambako amekuwa akipendekezwa na kushauriwa na waumini agombee nafasi hiyo.....

Walianza waumini wa msikiti mkuu wa Ijumaa wa Arusha alipokuwa kwenye ziara mkoani humo ambapo muumini mmoja alisimama na kusema kwamba kwa mawazo yake anaona Ponda anafaa kugombea nafasi ya urais kwa vile anaamini kuwa uwezo wa kuongoza anao..

Alisema mbali na uwezo pia yuko makini katika kusimamia jambo lolote lenya maslahi kwa waislam na kwamba mtu wa namna hiyo atafanya vyema zaidi akipewa dhamana ya kuongoza nchi....

Inaelezwa kuwa Ponda alipotembelea Zanzibar alipata wakati mgumu wa kuwakataa waislam waliojitokeza kumlaki katika misikiti ya Mpendae na Mbuyuni ambako alifanya mihadhara na kupendekezwa kugombea urais kwa kura nyingi na waumini ....

Kufuatia kusikika kwa mapendekezo hayo,Kisiwa lilimtafuta Ponda ili kusikia maoni yake juu ya maombi ya waislam kumtaka agombee urais.

"Sikuwa na fikra hiyo hata mara moja,lakini maadam limeletwa nami ni kiongozi wa taasisi ninawashukuru waliofikiria hivyo...

"Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote kuhusu hilo, ntalifikisha katika taasisi na maulana ndio watakaolitazama na kutoa uamuzi." Alisema Sheikh Ponda

Ponda alisema kuwa inawezekana waumini wakawa na mtazamo huo lakini viongozi wakawa na mtazamo tofauti kabisa,hivyo akawataka waumini kuwa na subira katika hilo.

-KISIWA.

No comments:

Post a Comment