NA ELIPHACE MARWA
JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania Mh. Fakih Jundu amewaasa waandishi wa habari kuwa makini pindi wanapo andika habari zinazohusu mahakama ili kuondokana na tatizo la kuingilia uhuru wa mahakama.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Jaji Kiongozi Fakih alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la kila wiki linalotuhumu muhimili huo kwa kushindwa kuwachukulia hatua stahiki watuhumiwa wa kesi za madawa ya kulevya.
"Huku ni kutaka kupambanisha wananchi na mahakama yao ambayo wana imani nayo, ni vyema waandishi kupata ufafanuzi wa kina wa mambo mbalimbali kabla ya kuandika habari isiyo ya kweli na yenye lengo la kupotosha Umma", alisema Jaji Fakih.
Aidha Jaji Fakih aliongeza kuwa ni vema kwa waandishi wa habari kuwa makini na uandishi wa habari zinazohusu mahakama kwa kuwa na ushahidi wa kutosha kwani kwenda kinyume na hapo ni kuingilia uhuru wa mahakama na si vizuri kwa waandishi wenye ueledi kuandika habari kwa ushabiki.
"Mengi ya mashauri yaliyotajwa na gazeti hilo bado yako mahakamani hivyo si vyema kuingilia uhuru wa mahakama hivyo habari hii inapaswa kukemewa kwa kosa la kuzungumza mambo yaliyo mahakamani", aliongeza Jaji Fakih.
Akizungumzia suala la kuwepo mahakama maalumu zitakazosimamia kesi za dawa za kulevya Jaji Kiongozi huyo amesema kama itaundwa na kuwezeshwa vizuri zinaweza kufanya kazi ila kama hazitawezeshwa kwa kupatiwa fedha na rasilimali watu hazitaweza kufanya kazi ipasavyo.
No comments:
Post a Comment