Tuesday, September 17, 2013

MWALIMU ANASWA AKIWAFANYIA WANAFUNZI MTIHANI WA DARASA LA SABA HUKO IRINGA

Jeshi la polisi mkoani Iringa linamshikilia mwalimu wa shule ya msingi Makungu wilaya ya Mufindi Bw Edwin Ambukile kwa tuhuma za kuwasaidia majibu wanafunzi wa darasa la saba katika mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Bw Ramadhan Mungi (pichani) amesema kuwa tukio hilo limetokea Septemba 15 mwaka huu.

Alisema kuwa mwalimu huyo ambae ni mwalimu wa masomo ya Sayansi katika shule hiyo pia alikuwa ni mwalimu wa masomo ya ziada ( katika shule hiyo na sababu ya kuwasaidia wanafunzi majibu ni kutaka kupata umaarufu kwa wanafunzi watano aliokuwa akiwafundisha masomo ya ziada aliopata kuwaahidi kuwa watafaulu mtihani huo. 

Alisema kuwa mwalimu huyo tarehe 11 septemba alipokea mitihani kutoka kwa msimamizi na baada ya hapo akafungua bahasha ya masomo ya Sayansi na kuanza kufanya mwenyewe na majibu kuyatuma kwa Sms kwa mke wake . 

Hata hivyo siku ya mtihani mmoja kati ya wanafunzi waliopata majibu hayo alipoingia katika chumba cha mtihani alionekana akitetemeka kupita kiasi na hivyo msimamizi wa mitihani alipompekua alimkuta na majibu hayo na kueleza jinsi alivyosaidiwa na mwalimu huyo .

Kamanda wa polisi alisema siku ya mtihani mwalimu Ambukile alipangiwa kusimamia shule ya msingi Igomaa na sasa amekamatwa na atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa