Thursday, September 26, 2013

NIMEKOMA BAADA YA FUMANIZI

SHETANI anazidi kuiatamia dunia, ulimwengu unawayawaya! Jamaa mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Manfree, mkazi wa Kimara Mwisho, Dar ambaye inadaiwa ni mfanyabiashara wa baa iliyopo Mbezi Mwisho (Mbezi Shamba) anadaiwa kunaswa na mke wa mtu (jina tunalo), Risasi Mchanganyiko linaibumburua.
Manfree baada ya kunaswa na mke wa mtu gesti.

Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lililoongeza faraja na furaha ya shetani kule kuzimu, lilijiri juzikati huko Kimara Mwisho ndani ya gesti moja (jina lipo kwenye droo zetu).
Mtuhumiwa akiomba msamaha kwa mwenye mke.

ALIYENASA AANZA KUMWAGIKA
Akizungumza kwa uchungu mkubwa, mume wa mwanamke huyo ambaye hakupenda jina lake liupambe ukurasa huu, alisema siku nyingi Manfree amekuwa akimsumbua mke wake, hali iliyokuwa ikimpa wakati mgumu mwanamme huyo mwenye mke.
“Jamaa amekuwa akimsumbua sana mke wangu, nilipokuja kuzipata taarifa hizi nilishangaa sana lakini pia niliumia kama mwanamme,” alisema mwenye mke huyo.
Mwenye mke (kushoto) akiongea na mke wa mtuhumiwa.

MAZOEA YALIPOANZA
Kwa mujibu wa mume huyo, kufahamiana kwa Manfree na mkewe kulikolea zaidi baada ya mwanamke huyo kuhitaji fremu kwa ajili ya biashara ya duka ambapo kwa kutumia uenyeji wa jamaa huyo, alionesha kutaka kumsaidia.

SINEMA YA KUNASWA ILIPOANZA
Mwanamme huyo aliendelea kusema kuwa sinema ya kunaswa kwa mwanamme huyo ilianza siku moja baada ya yeye kwenda kwenye baa ya jamaa huyo kuangalia mpira (hakuzitaja timu).
Alisema akiwa hapo baa, mara mke wake alitokea na kukaa kwenye kiti, meza nyingine. Jamaa huyo naye akaenda kukaa na mke wa jamaa na kuanza kuzungumza.
Nguo za Manfree zikiwa zimetundikwa chumbani.

“Mimi sikujua walichokuwa wakikizungumza na wala sikuwa na wasiwasi kwa vile jamaa ananifahamu, anafahamu yule ni mke wangu na anawafahamu hadi watoto wangu,” alisema mwanamme huyo.
Akaongeza: “Tulipofika nyumbani, mke wangu akasema amesikia mimi nina wanawake wengi nje, nimewafungulia biashara na mambo mengine kibao.
“Nilimuuliza ameambiwa na nani, akawa anagomagoma kunijibu lakini nilipombana sana mwisho akamtaja jamaa. Kumbe alipokaa naye pale baa ndiyo alikuwa akimwambia uongo huo.
“Mke wangu akaongeza kusema kuwa jamaa huyo kwa muda mrefu amekuwa akimtaka wakutane ‘praiveti’ lakini yeye amekuwa akimkatalia kwa sababu analinda heshima ya ndoa yake.
“Mke wangu alinionesha meseji ambazo jamaa alikuwa akimtumia, niliumia sana. Kwa kweli inauma sana jamani hasa kitendo hicho kufanywa na mtu ambaye mnafahamiana!”

MTIRIRIKO UNAENDELEA
Kwa mujibu wa mwanamme huyo, hali hiyo iliendelea kuisumbua ndoa yake huku maneno ya Manfree yakizidi kumvuruga kichwani.
SINEMA KAMILI HII HAPA SASA
Mume huyo alizidi kueleza kuwa baada ya mkewe kukiri kwamba Manfree amekuwa akimtaka wakutane chemba ndipo kwa pamoja walikubaliana kuandaa fumanizi.
“Nilimwambia mke wangu lazima tutege fumanizi, lengo ni kumfanya jamaa aachane na tabia hizi ambazo zinaweza kuharibu ndoa, watoto wakateseka na mambo menginemengine. Nilimruhusu amkubalie kukutana gesti,” alisema mume.

PICHA LINAKOLEA
Mume anasema siku ya tukio, Manfree bila kujijua alimtumia meseji mwanamke huyo, akamuomba wakutane ndani ya gesti moja iliyopo Kimara Mwisho ambapo bila kupoteza muda mwanamke huyo alimtonya mumewe juu ya meseji hiyo.
“Baada ya kunionesha meseji hiyo nilitafuta baadhi ya marafiki zangu ili twende pamoja kwenye eneo la tukio wakawe mashahidi.”
UTAMU ZAIDI
Baada ya mke kufika ndani ya gesti hiyo, mume anadai alimtaarifu jamaa huyo ambaye alitokea na kumwambia mwanamke huyo kuwa amuongezee shilingi elfu kumi kwani chumba ni elfu ishirini.

CHUMBANI ZAIDI
Kwa mujibu wa mume huyo, baada ya wawili hao kuingia chumbani humo, jamaa huyo alivua nguo zote na kukimbilia bafuni. Nyuma, mwanamke huyo aliutumia mwanya huo kumtaarifu mumewe ambaye naye aliwashika masikio marafiki ili wakae mkao wa kumnasa jamaa huyo.
Muda mfupi baadaye, mume anasema Manfree alitoka bafuni na kufikia kitandani puu! Hana hili wala lile, mwanamme huyo akiwa na ‘skwadi’ yake walizama ndani, wakagonga mlango, Manfree akakaribisha, alijua ni mhudumu amemletea bia maana aliagiza.
Mume alizidi kusema kuwa jamaa alipigwa butwaa na kuonekana kuweweseka. Yeye akamuuliza imekuaje yuko na mke wake chumbani? Jamaa akawa hana la kujibu.
MAELEZO YA KWENYE VIDEO
Katika maelezo yaliyomo kwenye video ya tukio zima (ipo chumba cha habari Global), Manfree anajieleza akimuomba msamaha mume huyo pamoja na wote waliokuwa chumbani humo.

MKE WA MANFREE AITWA
Mwanaume huyo anadai kuwa kwa hasira aliamua kumpigia simu mke wa Manfree ili afike kwenye gesti hiyo kushuhudia mumewe alivyokutwa na mke wa mtu gesti.
Anasema: “Mke alifika, akamkuta mumewe hajavaa nguo, aliumia sana lakini hakuwa na la kufanya.”
JAMAA KIZIMBANI
Baada ya ‘mhangaikaji’ wetu kuzipata data hizo, juzi asubuhi alimtafuta Manfree kwa njia ya simu ya mkononi kupitia namba alizopewa na watu wa karibu. Mwanzoni jamaa huyo alionekana kugoma lakini baada ya kubanwa kwa vielelezo alikubali huku akisema japo alinaswa lakini pia jamaa hao walitumia njia za kumteka.
“Aa..! Ni kweli nilikutwa na zahama hiyo lakini jamaa waliniteka bwana. Hata hivyo, sitarudia tena kuwa na uhusiano na wake za watu na tulishamalizana na mwenye mke kwa kumuomba msamaha,” alisema Manfree.
MKE WA MANFREE
Katika hali ya kushangaza, baada ya mkewe kupigiwa simu na mwandishi na kukiri kuwa ni kweli mumewe alinaswa chumba cha gesti akiwa na mke wa mtu, alisema bado anampenda na kwamba ndoa yao bado iko imara kama mizizi ya mti wa mbuyu!
“Ni kweli mume wangu alifumaniwa lakini bado nampenda sana na siwezi kumwacha, nitamvumilia maana ni mume wangu,” alisema mke wa Manfree aliyejitambulisha kwa jina moja la Sarah.
(Maneno yaliyotumika kwenye picha za ukurasa wa mbele, ni kama wanasema na si maneno halisi.)