Tuesday, September 10, 2013

Zanzibar yaapa kuishitaki meli iliyokamatwa na tani 30 za bangi Italia.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema itafungua mashtaka dhidi ya kampuni ya Gold Star, baada ya meli yake kukamatwa na tani 30 Za mihadarati aina ya bangi Kisiwa cha Malta Vessel, nchini Italia. 



Hatua hiyo ilitangazwa na Mkurugenzi wa Mamalaka ya Usafiri Baharini (ZMA), Abdi Omar Maalim, alipozungumza ofisini kwake Mlandege Zanzibar, jana. 


Maalim alisema kwa mujbu wa sheria namba 5 ya mwaka 2006 ya usafiri baharini, kampuni hiyo imekiuka masharti ya usajili, ambayo yanazuia meli kubeba silaha, dawa za kulevya, wakimbizi au mzigo wowote wenye biashara haramu. 


Alisema wanasheria wa ZMA wataipitia sheria hiyo kabla ya kuamua kuishtaki kampuni hiyo mabaharia tisa wanaodaiwa kula njma za kusafirisha bangi, kabla ya kukamatwa huko Italia. 


“Tunategemea kufungua mashtaka dhidi ya Kampuni ya Gold Star kwa kukiuka masharti ya fomu ya usajili, ambayo yanazuia meli kubeba mihadarati, silaha, wakimbizi au mzigo wowote haramu,” alisema Maalim. 


Alisema meli hiyo ilisajiliwa Oktoba 5, 2011 na Kampuni ya Uwakala wa Kusajili Meli ya Philtex Corparation yenye kituo chake kikubwa cha biashara nchini Dubai, inamilikiwa na raia wa Marekani na Phillipines. 


Maalim alisema Kampuni ya Philtex ina mkataba wa miaka 10 wa kusajili meli na SMZ, ikiwa na hisa asilimia 35 na SMZ 65. 


Alisema mkataba huo ulitiwa saini mwaka 2007 na umeweka sharti kuwa, hakuna kampuni yoyote yenye mamlaka ya kusajili meli kwa niaba ya SMZ zaidi ya kampuni hiyo hadi miaka 10 itakapoisha.


Alisema kulingana na mkataba huo, upande wowote utakaovunja masharti kabla ya muda kumalizika utalazimika kulipa fidia ya dola 500,000 za Marekani na kusisitiza kuwa, Philtex haina makosa kufuatia meli hiyo kukamatwa na bangi kwa vile ni uhalifu wa kawaida kama inavyotokea kwa meli nyingine.


Hata hivyo, Maalim alisema shehena hiyo ya bangi haieleweki hadi sasa kama ilikuwa ikisafirishwa kutoka Morocco au Uturuki na kwamba, mzigo huo haukutoka Tanzania kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Kuhusu Philtex kukumbwa na misukosuko ya usajili tangu kuanza kufanya usajili kwa niaba ya SMZ, Maalim alikiri mwaka jana meli 36 za Iran zilifutiwa usajili baada ya kubainika kusajiliwa kinyume na sheria za kidiplomasia

“Iran imewekewa vikwazo na Baraza la Usalama wa UN, zilifutiwa usajili wake baada ya kujitokeza malalamiko ya Zanzibar kusajili meli za mafuta za Iran,” alisema

No comments:

Post a Comment