Tuesday, January 27, 2009

MAUAJI YA ALBINO

Hatua ya viongozi wa serikali yetu kulizungumzia na kulikemea tendo hovu na la kinyama la mauaji ya ndugu zetu wa Kialbino linapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania. Kwa maoni yangu, tendo hili ni janga kubwa nchini mwetu na linastahili kila kipaumbele.
Inasikitisha sana kuona kwamba nchini mwetu bado tunao watu wenye imani pungufu za kishirikina/kichawi ambazo ndio chimbuko hasa la balaa hili. Yeyote anaeamini kwamba kwa kumchinja au kumjerui binadamu mwenziwe kwa minajili ya maendeleo yake kimaisha, basi mtu huyo hastahili kabisa kuwa kwenye jamii yetu na inabidi yeye ndie atokomee wa kwanza.
Wanaotenda matendo haya ya kinyama, si ajabu tunawajua kwani wanaishi nasi kwenye jamii na hatuna haja ya kuwafumbia macho na kuwaonea haya. Tuwafichue na sheria kali zichukuliwe zidi yao. Jamii nzima ni lazima iwaunge mkono Albinos, kwani hawa ni ndugu zetu awe kaka, dada, baba, mama, n.k. Hawakuchagua kuzaliwa hivo walivyo na hawana kasoro ya kusababisha kunyimwa haki zao za kuishi bila woga.
Ushirikina kamwe hautatuletea maendeleo, yawe kwa mtu binafsi, kundi la watu au nchi, bali ni juhudi na maarifa tuliyonayo. Tunaviomba vyombo vyote vya habari kuwa mstari wa mbele kwenye vita hii na viongozi wetu kuendelea kulikemea tendo hili.

No comments:

Post a Comment