Sunday, June 7, 2009

KUHUSU MJADALA WA UMOJA WA WATANZANIA NEW YORK.

Katika huu mjadala unaoendelea sasa hivi kuhusu kuundwa kwa umoja wa Watanzania Jijini New York ni vizuri tukawatazama wenzetu kutoka miji mingine na pande zote za dunia. Sisi ni wale wale na vigwezo tutakavyovitumia eti ndio sababu ya kutokuwa na umoja huo si vya ukweli. Makabila yaliopo hapa New York yako hata kwenye hiyo miji mingine na duniani kote, elimu nayo haiwezi kuwa sababu na wala shughuli anayoifanya mtu. Muhimu zaidi ni mshikamamo wa sababu za kimsingi za kuwa na umoja huo.


Watanzania siku zote tutabaki kuwa Watanzania na kwa kutambua hilo basi ni lazima tuelewe ya kuwa UMOJA ndio ngao yetu kubwa. Ukabila, udini, jinsia, elimu na mengi mengineyo hayana nafasi kwenye kuwatenganisha watoto wa Kambarage. Ikumbukwe ni kiasi gani Baba wa Taifa alijitolea mhanga kuujenga, kuulinda na kuutetea umoja wetu. Sasa iweje leo eti tushindwe kuwa wamoja kwa sababu ya ukabila, udini, elimu au kazi aifanyayo mtu?


Nia na madhumuni ya kuwa na umoja ni kujumuika na kusaidiana iwe wakati wa raha ua matatizo na pia kutizama maslahi yetu hapa ugenini. Kunapotokea misiba na sherehe siku zote kunahitajika watu na watu wenyewe ndio sisi. Na tulio wengi tumeanza familia huku ugenini na tuna hamu sana ya kuendeleza mila na desturi zetu kwa watoto wetu lakini pengine inatuwiha vigumu kwa sababu ya kile nitakochokieleza ya kwamba tupo tupo tu!!

Hakuna aliye bora kuliko mwingine. Sote hatuwezi kuwa sawa kimaisha lakini hadhi na ubinadamu wako siku zote utabaki pale pale. Maisha ni safari na sisi sote ni wasafiri kwenye basi moja, lakini lazima kuwe na watakao kaa mbele, katikati na nyuma ya basi. Utakapofika kwenye kituo chako utashuka na wengine watapanda.

Nawaimiza ndugu zangu Watanzania mnaoishi Jiji la New York tufanye jitihada za kuunda huo umoja haraka iwezekanavyo. Najua wako wengi wanaoniunga mkono kwenye hili jambo, na vile vile najua wako ambao wana sifa na vipaji vya uongozi. Naomba tujitokeze.
-Fundi Kombo-

2 comments:

  1. Umbeya unafiki na kunata kumezidi!

    ReplyDelete
  2. Haya lini mkutano nataka kujiunga.

    ReplyDelete