Monday, December 14, 2009

KUFUATILIA MAONI YANGU KUHUSU MIAKA 48 YA UHURU, MDAU MMOJA AJIBU KAMA IFUATAVYO:

Je, na wewe uliyeikimbia na kuitelekeza nchi tukuiteje? Wewe umeifanyia nini nchi hii? Baadhi ya viongozi wetu wamejaribu sana na baadhi ya sababu za kushindwa kwa sera zao ziko nje ya uwezo wao. Makosa yapo yametendeka lakini hawakukimbia nchi. Kama kweli una uchungu na nchi yako RUDI kwenu Tanga ukasaidie wazigua wenzio na siyo kukaa Malekani na kubakia kulalamika!
Happy 48th Birthday Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na usitishwe na vikaragosi na wasaliti. Safari ni lazima iendelee na tutafika tu!
Kwanza;Ningependa huyu ndugu akubali kwamba kama Mtanzania nina haki ya kutoa maoni yangu kwa jinsi nionavyo mimi na kwa kufanya hivyo hainifanyi mimi kuwa kikaragosi au msaliti kwa nchi yangu.
Pili; napenda kumkumbushia ndugu huyu ya kwamba kuna Watanzania wengi sana waishio nje ya Tanzania, na si kwamba wameikimbia na kuiteketeza nchi yao, bali kuna sababu nyingi za kimsimgi zinazowafanya wawe huko waliko, na baadhi ya hizo ni elimu, kazi, sanaa na nyingine nyingi. Hata uko waliko, wengi wao bado wanashiriki kikamilifu kwa namna mbalimbali kuliendeleza Taifa. Tulio wengi hutuma mapesa ya kigeni huko nyumbani na kuyaingiza kwenye mzunguko wa kiuchumi wa nchi hiyo tunayodaiwa kuisaliti.
Ndugu unaonekana kuridhika kabisa na hali nchini mwako hata kama itachukua miaka mingine 48 na wananchi kule vijijini wanaendelea kutaabika, nadhani kwako ni sawa kabisa kila mwaka kukiwa na mgao wa umeme, na ufisadi umeufumbia macho kabisa! Hao viongozi unaowasema wewe kwamba hawakukimbia nchi endelea kujilinganisha nao maana wao wakiugua watapelekwa hospitali ya Mwananyamala na sio Uingereza au Afrika ya Kusini. Ndugu acha kujidanganya, hao sio wenzako.
Wako viongozi waliokuwa na uchungu na nchi hii (Tanzania) na Baba wa Taifa ni mmojawapo. Walikuwa na sera zakutaka kumnufaisha kila Mtanzania ingawa kweli nyingine zilishindikana. Sasa hivi ni sera za kisiri siri... na siajabu ndizo hizo zinazotuletea matatizo ya nyingi ya rasilimali zetu kupotea bure. Hivi katika hiyo miaka 48, dhahabu, Almasi, Tanzanite, utalii vimetusaidia nini?
Ndugu kama unadhani bado tuna muda wa kufanya makosa na bado tukayaachia yaendelee basi endelea kuwaachia hao viongozi wako na sera zao za siri. Nahisi masuala muhimu ya nchi yataendelea kusainiwa na watu binafsi na maamuzi kufanyika na baadae ndio BUNGE la Wananchi kuyajadili baada ya kila kitu kuharibika.
Labda pengine tulio nje ya nchi inatusaidia kujifunza na kuona mengi na kuwa na uwezo wa kutofautisha. Unapokuwa kwenye choo pua huwa zinazoea harufu ya kinyesi na huwa haikubugudhi, tofauti na atakaeingia chooni hapo baada ya wewe kutoka! Ndugu nchini mwetu tuna matatizo! Fungua macho uone, tembea ujifunze... "Wao wanaweza kwa nini sisi tushindwe?" Yanayofanyika duniani kote hata Tanzania yanawezekana na si lazima tusubiri miaka mingine 48.
Ndugu yote haya nayasema kwa sababu nina uchungu sana na nchi yangu, na kwa kukutaarifu ni kwamba kila mwaka hufanya bidii ya kuja nyumbani Tanga kwa Wadigo wenzangu na kutaabika nao kwa jinsi nchi yetu inavyozidi kuyumba. Hivyo basi ndugu yangu ukae ukijua kukereketwa huku hakutokani na habari za kusoma magazetini au kuambiwa, bali ni kwa kuyaona mwenyewe. Tafadhali washauri hao viongozi wako watumie hizo pesa wanazotumia kusheherekea uhuru kila mwaka, ziende kwenye kuboresha elimu, kutokomeza malaria, kupeleka maji safi na umeme usio na mgao vijijini, na mengineyo ya msingi badala ya magwaride yasiyo na manufaa yo yote kwa watanzania. Tusheherekee mafanikio na sio failure!
-Fundi Kombo-