Friday, May 25, 2012

POLISI YAPIGA STOP MAANDAMANO YA CHADEMA

<><> <><>
JESHI la Polisi limepiga marufuku matembezi ya amani (maandamano) ambayo yameombwa kufanywa kesho na Chama Cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema).
Huku, jeshi hilo likibariki Mkutano wa chama hicho kufanyika kwenye viwanja vya Jangwani.
Polisi limefikia hatua hiyo, baada ya kubaini kuwa hakuna sheria yoyote inayoruhusu chama cha siasa kufanya matembezi au maandamano isipokuwa mkutano.
Mei 26 Chadema, kilituma maombi ya maandishi (barua) kwa jeshi hilo kuruhusu matembezi hayo ya amani, kutoka sehemu mbalimbali za jiji hadi viwanja vya Jangwani panapofanyika mkutano wa hadhara leo.
Lakini jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Afande Suleiman Kova alisema, “Hakuna sheria yoyote ya Uchaguzi inayoeleza chama cha siasa  kufanya matembezi, hivyo hatukubaliani na ombi lao lakini hili la mkutano ruksa kufanya hivyo”
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, Chadema iliwasilisha barua ya kuomba kibali cha kufanya mkutano, lakini kabla ya kujibiwa Mei 26 kiliwasilisha barua nyingine ili kupata kibali cha matembezi ya amani.
“Walisema wanachama wao hawana nauli, kutoka kwenye maeneo ya jiji kwenda viwanja vya Jangwani, lakini mbona jana walifika Mahakama Kuu kwa magari na mabasi, kwa hili hatuwezi kukubali”alifafanua.
Pia, polisi limesema mwanachama yoyote ambaye atapuuza amri hiyo, jeshi litamchukulia hatua za kisheria ikiwemo kukamatwa.
Kamanda aliwaonywa Wanachama kutodanganyika na wakuu wao wa chama kwa kufanya matembezi hayo, kwani jeshi linamchukulia hatua  za kisheria Mwananchi sio chama cha siasa.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, jeshi la polisi halipendi kuona amri zake zikipindishwa, au kugombana na vyama vya siasa.
Alienda mbali zaidi akisema, mji wa Dar es Salaam, unatakiwa kuwa na amani wakati wote, hivyo amri hiyo wana hakika itatekelezwa.
Kwa upande mwingine Kova, alionya juu ya Mkutano huo wa leo, akisema uwe wa amani na utulivu.
Alisema polisi wako tayari kutoa ulinzi wakati wote wa mkutano huo ili kuhakikisha kunakuwa na amani.

No comments:

Post a Comment