Tuesday, July 31, 2012

HASIRA ZA MKIZI FURAHA KWA MVUVI' NGASA SASA KUUZWA M 80

 


KLABU ya Azam Fc ya jijini Dar es Salaam, imetangaza katika ukurasa wake wa Facebook kumuuza mshambuliaji mahiri wa timu hiyo aliyejiunganao kwa dau kubwa akitokea Klabu ya Yanga, Mrisho Ngasa kwa dau la Dola za Kimarekani 50,000, ambazo ni sawa na Sh. milioni 80  za kitanzania.


Uongozi wa Klabu hiyo umeweka wazi kuwa umekasirishwa na kitendo cha mkali huyo kuonyesha mapenzi ya wazi kwa kuibusu Jezi ya Klabu yake ya zamani Yanga baada ya kuifungia timu yake bao lililoiwezesha kuipeleka timu hiyo hatua ya Fainali za Kombe la Kagame dhidi ya timu hiyo na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, wakati akishangili bao lake mbele ya jukwaa la mashabiki wa Yanga.


Katika Mchezo huo Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutinga hatua ya Fainali katika michuano hiyo, ambapo ilikutana na Yanga katika Fainali hizo mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo Ngasa, aliingia akitokea benchi katika dakika za mwisho za mchezo huo.


Azam imeonyesha kukasirishwa na kitendo hicho cha Ngasa na kukielezea kuwa hakikua sahihi, ambapo awali uongozi huo ulikaliliwa kuwa ulikichukulia kitendo hicho kama tukio la kimichezo zaidi kutokana na mchezaji huyo kuwa alifanya hivyo huku akiwa tayari ametimiza majukumu yake ya uwanjani na kuwafungia bao muhimu katika mashindano hayo, na kuongeza kuwa hawakuona vibaya kwa Ngasa kuonyesha furaha yake kwa kushangilia kwa staili yake aipendayo.


Lakini sasa Uongozi huo umekuwa na kauli tofauti kuhusu tukio hilo ambapo sasa kama walivyojieleza katika mtandao wao wa Facebook, kuwa wamekasirishwa na kitendo hicho kilichoonyeshwa na Ngasa.


Aidha Uongozi huo umesema kuwa upo tayari kupokea ofa yeyote kutoka kwa timu yeyote iwe ya ndani ya nchi au nje ya nchi kwa dau hilo walilolitaja. 


Uongozi huo ukionyesha hisia zake juu ya kukasirishwa huko, umeeleza kuwa mara kadhaa umemshuhudia Ngasa, akitinga katika Jengo la Klabu ya Yanga, kuwafuata rafiki zake Jerry Tegete, Hamis Kiiza na Niyonzima.


Mrisho Ngasa (kulia) akipozi kwa picha na Haruna Niyonzima, baada ya mchezo wa fainali za Kombe la Kagame uliozikutanisha timu zao jumamosi iliyopita, na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kutwaa Kombe la Kagame 2012 kwa mara ya pili mfululizo.

No comments:

Post a Comment