Friday, September 21, 2012

MAKABURI YA TANA RIVER YAFUKULIWA





Polisi na wataalamu wa kuchunguza maiti wamepigwa na mshangao mkubwa baada ya kukosa kupata chochote ndani ya makaburi ya siri yaliyogunduliwa katika eneo la Tana River.
Polisi walipewa amri ya kufukua makaburi hayo hii leo katika kijiji cha Ozhi ambako mapigano kati ya jamii za Orma na Pokomo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu miamoja na kuwaacha maelfu bila makao.
Kwa mujibu wa naibu kamishna wa polisi eneo la Tana River, Anthony Kamitu, makaburi hayo yalikuwa na mitaro minne ishara kuwa watu walikuwa wamezikwa kwenye makaburi hayo. Ingawa bwana Kamitu alisema kuwa hawakupata miili yoyote licha ya kuwa kulikuwepo na harufu mbaya ishara kwamba maiti waliokuwa ndani ya makaburi hayo waliondolewa. Bwana Kamitu anasema kuna hofu kuwa wahalifu kutoka jamii ya Pokomo waliitoa hiyo miili kwenye makaburi hayo huku polisi wakisubiri kibali cha mahakama ili kuweza kuyafukua. Polisi wamefahamisha BBC kuwa makaburi hayo yalikuwa tu na mguu mmoja wa kushoto wa mtu na wanashuku kuwa maiti waliokuwa ndani ya makaburi hayo waliondolewa na kupelekwa kwingineko.

Zaidi ya watu miamoja wamefariki katika mapigano kati ya jamii hizi mbili ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda wa mwezi mmoja ulipita. Makabiliano kati ya jamii hizo mbili yalianza katikati ya mwezi jana na kusababisha mashambulizi ya kuvizia na ya kulipiza kisasi.

Chanzo: http://www.bbc.co.uk/swahili

No comments:

Post a Comment