Friday, September 21, 2012

NANI KUBEBA 1.5 LEO UKO TMK



Na Princess Asia
SHINDANO la kumsaka mlimbwende wa Kanda ya Temeke, Miss Temeke 2012 linafanyika leo katika ukumbi wa PTA, Sabasaba, Dar es Salaam na mshindi atazawadiwa Sh. Milioni 1.5 mbali na tiketi ya kushiriki Miss Tanzania baadaye mwaka huu.
Benny Kisaka, Mkurugenzi wa BMP Promotions, waandaaji wa Miss Temeke 2012, aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, katika mlolongo huo wa zawadi, mshindi wa kwanza atajinyakulia fedha taslim Sh. Milioni 1.5, wa pili Sh. 800,000, wa tatu Sh. 700,00 sambamba nguo ya kutokea jioni na viatu, vyenye thamani ya Sh. 500,000 kila mmoja kwa wote watatu.
Kisaka alisema kwamba duka la kisasa la Mariedo Boutique itatoa gauni la Sh.350,000 na kiatu cha Sh 150,000 kila mmoja kwa washindi hao watatu wa kwanza watakaoshinda. Alisema mbali ya washindi hao, mshindi wa nne atajinyakulia kitita cha Sh. 400,000 ambapo mshindi wa tano ataondoka na Sh 300,000 wakati warembo wengine wote watakaosalia kila mmoja atapata Sh.200.000.
Ikiwa ni funga dimba ya mashindano ya urembo ya kanda nchini, shindano hilo litanogeshwa na wasanii wanaong’ara katika luninga, Mpoki wa kundi la Orijino Komedi na Steve Nyerere ambaye mbali ya kuigiza sauti za watu mbalimbali, pia ametoa filamu kadhaa kwa siku za hivi karibuni.
Mbali ya wasanii hao, bendi ya Mashujaa Musica, yenye wanamuziki nyota kama Charles Baba, MCD, Ferguson, Ali Akida na wanennguaji kama Lillian Internet na wengineo pia itanogesha usiku huo.
Taji la Miss Temeke, linashikiliwa na Husna Twalib na washiriki walikuwa wakijifua kwa wiki tatu chini ya mkufunzi, Leilla Bhanji, ambaye amekuwa akisaidiwa pia na warembo wa miaka ya nyuma wa Miss Temeke akiwemo, Regina Mosha (2002, Hawa Ismail 2003), washiriki wa mwaka jana Joyce Maweda, Mwajabu Juma, Cynthia Kimasha na katika shoo wamekuwa na Dickson Daud kutoka kundi la THT.
Shoo ya ufunguzi itakuwa tofauti kabisa na shoo nyingine yeyote iliyowahi kuyanyika nchini, kwani imezingatia zaidi urembo na nini msichana anatakiwa kufanya na si unenguaji tu. Warembo 15 wanatoka katika vitongoji vya Kigamboni, Kurasini na Chang'ombe ambapo kila sehemu wametoka warembo watano ambapo washindi watatu wa kwanza watapata fursa ya moja kwa moja kushiriki Redds Miss Tanzania 2012.
Warembo hao ni Agness Goodluck, Angela Gasper, Flaviana Maeda,Edna Sylvester, Catherine Masumbigana, Khadija Kombo, Neema Doreen, Flora Kazungu, Lilian Joseph, Elizabeth Peter, Elizabeth Boniphace, Jesca Haule, Zulfa Bundala, Mariam Ntakisivya na Esther Albert.
Temeke inajivunia kutwaa taji la Miss Tanzania mara tatu, kupitia warembo Happiness Sosthenes Millene Magesse mwaka 2001, Sylvia Remmy Bahame mwaka 2003 na Genevieve Mpangala mwaka 2010.
Lakini pia imetoa warembo waliowahi kushika nafasi ya pili na tano bora katika Miss Tanzania kama Jokate Mwegelo, Irene Uwoya, Irene Kiwia, Queen David, Cecylia Assey, Sabrina Slim, Miriam Odemba, Ediltruda Kalikawe na Asela Magaka.


Edna Sylvester (21)



Catherine Masumbigana (21)  

Jesca Haule (18)

Lilian Joseph (20)

Neema Doreen (20)

Zulfa Bundala (21)

Esther Albert (19)

Agness Goodluck (20)

Flaviana Maeda (22)

Elizabeth Peter (21)

Miriam Ntakisivya (21)


Elizabeth Bonigace (19) 


Angel Gasper (19)

No comments:

Post a Comment