Friday, September 14, 2012

WAZIRI WA UJENZI DK JOHN MAGUFULI AWACHIMBA MKWARA MAKANDARASI WA UJENZI WA DARAJA LA KIGAMBONI


 Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli (katikati), akikagua ujenzi wa daraja la Kigamboni akiwa ameambatana na viongozi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki (mwenye shati jeupe kulia), Mbunge wa Kigamboni Dk Faustine Ndugulile (wa pili kulia) leo jijini Dar es Salaam. Daraja la Kigamboni linajengwa na Kampuni ya China Railways Engineering kwa gharama ya shilingi bilioni 214 na linatarajia kukamilika kabla ya mwaka 2015.
 Daraja la Kigamboni likiendelea kujengwa katika bahari ya Hindi eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam. Daraja hilo litakapokamilika litakuwa na njia 6 pamoja na barabara za juu na kuwa moja ya Daraja kubwa na la kipekee Afrika Mashariki na Kati.
Msafara wa Waziri wa Ujenzi, John Magufuli ukipita katika daraja  la awali litakalotumika kupitishia vifaa vya ujenzi wa daraja la Kigamboni katika eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam juzi, wakati walipofanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo. Daraja hilo litajengwa na Shirika la Taifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Serikali ya Tanzania


DAR ES SALAAM, Tanzania
WAZIRI wa Ujenzi, Dk.  John Magufuli amewaonya Makandarasi na Mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuwa watajibishwa kwa uzembe wowote, huku akimtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi wa daraja la Kigamboni, kuhakikisha linakamilika kabla ya Rais Jakaya Kikwete hajaondoka madarakani.

Magufuli alitoa onyo hilo leo jijini Dar es Salaam, kwenye ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya barabara pamoja na kupokea ripoti ikiwamo ya daraja la Kigamboni na kusema; “Mkataba wa kukamilika daraja hili ni miezi 36, hivyo mkandarasi ufanye juu chini daraja hili likamilike kabla ya Rais Kikwete hajatoka madarakani na alizindue yeye,” alisema.

Kwa upande wake, Injinia Karim Mattaka, alisema ujenzi wa daraja la Kigamboni utakuwa ni wa pekee, kwani litakuwa la kwanza kwa nchi ya Afrika kutokana na kampuni ya ukandarasi inayosimamia kubobea katika ujenzi wa madaraja ya aina hiyo.


akisisitiza ubora wa kazi, Dk Magufuli alisema kuwa, wizara yake ipo makini na kuwataka makandarasi kufanya kazi kwa usanifu mkubwa na wakichemka watawajibishwa kama ilivyokuwa kwa mkandarasi wa barabara ya Kilwa.

“Nasema makandarasi wajue kuwa Tanzania si sehemu ya kujifunzia kazi, atakayefanya vibaya itamgharimu mwenyewe kwa kurudia ujenzi kwa gharama zake na hata kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Kuanzia sasa, makandarasi watakaojenga chini ya kiwango watawajibishwa kwa kufukuzwa kazi mara moja na adhabu nyingine,” alisisitiza Magufuli.