Thursday, January 31, 2013

BALOZI IIDI AWAJULIA HALI WALIONUSURIKA KIFO KATIKA AJALI YA JAHAZI LILILOKUWA LIKITOKEA TANGA KWENDA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akimfariji mmoja kati ya abiria waliokua katika Jahazi la Sun Rise, Juma Ali Jaku , iliyopata ajali na kuzama kati ya Tanga na Mkokotoni karibu na Mkondo wa Nungwi, ikiwa imebeba jumla ya abiria 32 kati ya hao 21 wameokolewa na 11 kati yao hadi sasa hawajapatikana. Kushoto kwa Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pemba Juma Khamis.
Nahodha wa Jahazi ya Sun Rise, iliyozama kati ya Tanga na Mkokotoni, karibu na Mkondo a Nungwi, Abdulla Saleh, akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, jinsi mkasa huo ulivyowatokea na kuzama baada ya chombo chao kupatwa na dhoruba kali.
**************************************

Nahodha na abiria mmoja ambao ni miongoni mwa watu 21 walionusurika kufa kati ya 32 waliokuwa wakisafiri na Jahazi lililopata ajali na kuzama liitwalo Sun Rise likitokea Mkoani Tanga kuja Mkokotoni Unguja, wakiwa katika wodi ya Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini A iliyopo Kivunge, Zanzibar wakiendelea kupatiwa matibabu.
Jumla ya abiria 21 wameokolewa katika ajali hiyo na kupelekwa Kivunge kwa ajili ya kupatiwa huduma ya matibabu ambapo hadi sasa abiria saba watoto wakiwa watatu na watu wazima wane bado hawajapatikana kutokana na ajali hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Viongozi wa Juu wa Ofisi yake ambayo ndio inayoratibu masuala ya maafa walifika Hospitali ya Kivunge kuwapa pole majeruhi hao waliobakiwa wakipatiwa huduma za Matibabu.
Nahodha wa Jahazi hiyo Bwana Abdulla Saleh akiwa pamoja na Majeruhi mwenzake Bwana Ali Juma Jaku alimueleza Balozi Seif kwamba ajali hiyo ilitokea kutokana na kuchafuka mara Moja hali ya Bahari.
Nahodha Abdulla alisema chombo chao chenye uwezo wa kubeba abiria 50 kiliondoka bandarini Tanga salama Majira ya Saa nane za Usiku na walianza kupata mitihani na kuzama mara baada ya kuchafuka kwa bahari majira ya saa 11 za alfajiri.
Akiwapa pole majeruhi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar Balozi Seif alisema juhudi alizoonyesha Nahodha huyo katika kusaidia uokozi huo zinastahiki kupongeza na Jamii yote.
Balozi Seif aliwaombea majeruhi hao kupoa haraka na kuungana na familia zao na kuutaka Uongozi wa Hospitali ya Kivunge kuendelea kuwachunguza Mareruhi hao kutokana na juhudi kubwa waliyoifanya ya kusaidia harakati za uokozi wa wenzao uliopelekea kupoteza nguvu nyingi.
Jahazi hilo la Sun Rise lililokuwa likitokea Tanga kuja Mkokotoni mbali ya kuchukuwa abiria pia lilibeba sanduku nne za maziwa pamoja na Polo zipatazo 30 za Mkaa.
Othmna Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
31/1/2013.

No comments:

Post a Comment