Tuesday, January 8, 2013

UJENZI WA CHUMBA CHA CHINI YA BAHARI WAZINDULIWA NA BALOZI IDDI-PEMBA


Chumba cha chini ya Bahari kikionekana kwa mbali kikiendelea na matengenezo kwenye Hoteli ya Manta Resort Makangale iliyoko Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, akishusha Nanga kuashiria kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chumba cha chini ya bahari katika Hotelai ya Manta Resort, iliyoko Makangale Kaskazini mwa Kisiwa cha Pemba jana.
Meneja wa Hoteli ya Manta Resort Makangale mkoa wa kaskazini Pemba Bwana Metthew Saus {maarufu kama Babu kwanini) na msaidizi wake wakiwa tayari kumsubiri mgeni rasmi Balozi Seif Ali Iddi kuweka jiwe la Msingi na Nanga katika ujenzi wa chumba cha chini ya bahari.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa na Mkewe Mama Pili Seif Iddi, wakiwa kwenye Boti kuelekea kwenye uwekaji wa jiwe la msingi na nanga ya ujenzi wa chumba cha chini ya bahari katika Hoteli ya Manta Resort iliyoko Makangale Mkoa Kaskazini Pemba.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Pili Seif Iddi akijigeza moja ya kanzu zilizotengenezwa na wajasiri amali wa Jimbo la Gando ambayo aliondoka nayo kwa manunuzi.
Balozi Seif akiwa na Mkewe Mama Pili Seif Iddi wakifuaria bidhaa zilizotengenezwa wajasiri amali wa Jimbo la Gando huku wakipata maelezo kutoka kwa mjasiri amali wa kikundi hicho Bibi Faida Hamad Juma.



Wajasiri amali hao walipata futrsa ya kutangaza bidhaa zao katika hafla ya uwekaji wa jiwe la nanga la ujenzi wa chumba cha chini ya bahari hapo Manta Resort Makangale Kaskanzini mwa kisiwa cha Pemba. Picha na Hassan Issa wa – OMPR- ZNZ.
**********************************

Harakati za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Sekta ya Utalii zimeanza kuonyesha dalili za mafanikio kufuatia uwekezaji wa daraja la juu katika sekta hiyo kuanza kushamiri kidogo kidogo hapa Nchini.
Ujenzi wa chumba cha chini ya bahari { under water room} ulioanzishwa kama mradi maalum wa kuvutia watalii wa daraja la kwanza unaofanywa na Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort iliyopo Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba ni miongoni mwa dalili hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikuwa mgeni rasmi katika uwekaji wa jiwe la nanga la ujenzi wa chumba hicho kitakachokuwa chini ya Bahari ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif akiambatana na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Wizaraya ya Habari wakiwemo maafisa wa sekta ya Utalii na wanasiasa alionekana kufarajika na mradi huo mpya ndani ya Bara la Afrika na ni wa pili kufanywa Duniani ukitanguliwa na ule wa Sweden ulioko katika maji ya ziwa.
Akizungumza katika hafla hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema ni jambo la kutia moyo kuona Kisiwa cha Pemba hivi sasa kinanza kupanuka Kiutalii kufuatia kuimarika kwa miundombinu iliyowekwa.
Aliwataka wananchi wa Kisiwa cha Pemba kuchangamkia sera ya Utalii kwa wote kwa lengo la kuitumia fursa hiyo adhimu kabla haijavamiwa na wafanyakazi wa nje ya Visiwa hivi.
‘’ Pemba sasa ni eneo ambalo Serikali inaliangalia katika kufunguka kiutalii hasa kutokana na kukamilika kwa miundombinu ya umeme na Bara bara’’. Alifafanua Balozi Seif.
Alikumbusha kwamba Zanzibar bado haijatangazwa kiutalii nje ya Nchi na watu wanaofikia hatua za kufanya hivyo huitangazia kwa maslahi yao binafsi.
Balozi Seif ameiagiza Taasisi inayosimamia uwekezaji vitega uchumi Zanzibar { ZIPA } kuziangalia upya sheria zilizopo za uwekezaji ili kuwepuka kurejea makosa yaliyojitokeza tokea kuimarishwa kwa sekta ya Utalii Nchini.
Alisema ipo miradi ya uwekezaji ambayo imekuwa mtihani kwa serikali kwa vile imeshindwa kutoa huduma zilizokusudiwa akiutolea mfano mradi wa Hoteli ya Mawimbini ambao kmwa sasa umeshindwa kufanya kazi.
Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema mradi huo wa chumba cha chini ya Bahari masafa ya Mita 100 ni wa majaribio.
Mh. Said alieleza kuwa mradi huo wa chumba kimoja utakapofaulu Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort umekusudia kujenga vyumba vingi zaidi ili kufanikisha utali wa daraja la juu.
Mapema Meneja wa Hoteli ya Manta Resort Makangale Bwana Metthew Saus Maarufu kwa jina la Babu kwa nini alisema wazo la ujenzi wa mradi huu lilichukuwa takriban miaka saba kwa kufanywa utafiti chini ya bahari.
Babu kwani alisema Kisiwa cha Pemba kina mazingira mazuri ya kuendeleza mradi huo ikilinganishwa na mradi wa mwanzo Duniani kama huo ulioanzishwa Nchini Sweden.
Amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kusherehekea miaka 49 ya mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 yaliyowatoa katika makucha ya wakoloni.
Mradi huo wa chumba cha chini ya Bahari unaokisiwa kugharimu Dola za Kimarekani Laki Tano sawa na Shilingi za Kitanzania Milioni Mia 758,000,000/- utakamilika rasmi ndani ya muda wa siku Tisini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/1/2013.

No comments:

Post a Comment