Saturday, January 5, 2013

WAFADHILI WA MAENDELEO WATAKIWA KUCHANGIA HUDUMA ZA AFYA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi Muuguzi Mkunga wa Wodi ya Watoto waliopata ajali Bibi Leluu Omar Said msaada wa vitanda 14, magodoro na mashuka yake kwa ajili ya wodi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwakagua watoto waliolazwa kupatiwa huduma katika wodi ya ajali Mnazi Mmoja kabla ya kukabidhi msaada kwa ajili ya wodi hiyo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkagua mmoja wa wagonjwa wa wodi ya Mifupa aliyelazwa kabla ya kukabidhi msaada wa vifaa vilivyotolewa na wasamaria wema.

Wafadhili na washirika wa Maendeleo wameendelea kukumbushwa kuchangia huduma za afya kwa nia ya kuwaondoshea mzigo wananachi pamoja na Serikali katika upatikanaji wa huduma hiyo muhimu. 
Kumbusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akikabidhi Msaada wa Vitanda 28 pamoja na Magodoro, Mito na mashuka yake kwa ajili ya Wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Msaada huo wa Vitanda unaokadiriwa kugharimu shilingi za Kitanzania Milioni 12,000,000/- unazihusu wodi ya Watoto wanaopata ajali, Wodi ya Mifupa ya wagonjwa wa Kiume pamoja na chumba wanacholazwa wagonjwa wanaotumikia chuo cha mafunzo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Akikabidhi msaada huo uliotolewa na Wasamaria wema Balozi Seif alisema bado Hospitali pamoja na Vituo vya afya hapa Nchini vinahitaji kupatiwa misaada ili viweze kutoka huduma katika kiwango kinachokubalika.
Alifahamisha kwamba Serikali kwa upande wake itaendelea kujitahidi zaidi katika kutafuta wafadhili sambamba na kuongeza nguvu za upatikanaji wa vifaa vya huduma lengo likiwa ni kuimarisha huduma za afya mijini na Vijijini.
Msaada huo unafuatia ziara yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyoifanya katika sekta ya afya mwaka uliopita na kushuhudia changamoto kadhaa zinazovikabili vituo vingi vya afya pamoja na Hospitali ukiwemo uhaba na uchakavu wa vitanda na magodoro ya wagonjwa.
Wakipokea msaada huo kwa nyakati tofauti Muuguzi Mkunga katika wodi ya Watoto Bibi Leluu Omar Said na Muuguzi dhamana katika Wodi ya Mifupa ya Wagonjwa wa Kiume Bibi Afsa Abdulla wamewashukuru wafadhili hao kupitia Balozi Seif kwa msaada wao utakaosaidia kupunguza matatizo yanayozikabili hospitali hiyo.
Wauguzi wakuu hao wa wodi hizo wameahidi kwa pamoja kuvitunza Vifaa hivyo ili vidumu kwa muda mrefu kwa vile changamoto hilo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu.
Hata hivyo wauguzi hao wameiomba serikali kufanya utaratibu wa hifadhi zaidi ya magodoro hayo ili yadumu zaidi suala ambalo Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya kulifanyia kazi mara moja.
Mapema Balozi Seif alipata fursa ya kuwakagua waonjwa waliolazwa katika wodi zilizofanikiwa kupata msaada wa Vitanda, magodoro pamoja na Mashuka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kutoa msaada kama huo hivi karibuni katika Hospitali za Micheweni na Vitongoji Kisiwani Pemba.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
5/1/2013.