Na Anna Nkinda – Maelezo
Wazazi nchini wametakiwa kuwafundisha watoto wao kazi zote za nyumbani bila ya kuwabagua kwamba hawa ni watoto wa kike na hawa ni watoto wa kiume hiyo itawasaidia kuweza kujitegemea hasa wanapokuwa katika mazingira ya tofauti na nyumbani.
Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipotembelea ofisi za makao makuu ya Chama cha Girls Guide zilizopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mlezi wa chama hicho alisema kuwa hivi sasa wanawake wanatakiwa kuondokana na mfumo dume kuwa ukiwa na watoto wa kike na wa kiume ndani ya nyumba kazi zote zinatakiwa kufanywa na mtoto wa kike pekee.
“Mzazi unatakiwa kuhakikisha kuwa watoto wako bila ya kuangalia jinsia wanafanya kazi sawa sawa kama ni kupika leo iwe zamu ya huyu na kesho zamu ya mwingine hii itamsaidia mtoto wa kiume akienda shule ya bweni kukumbuka kuwa nyumbani nilikuwa naosha kikombe, nadeki nyumba, nafua nguo, nashona kifungo na kuweza kufanya mwenyewe.
Lakini leo hii mtoto wa darasa la saba hawezi kufanya kazi yoyote ya nyumbani kwani hata mama yake naye hana muda wa kumfundisha”, alisema Mama Kikwete.
Alisema kuwa kama wakiwafundisha watoto vizuri kutokana na muongozo uliopo katika madarasa ya boy skauti na girl guide watakuwa wamewakomboa hata kama siyo wote lakini wale wachache ambao hawakupata mafunzo nyumbani watapata mazingira ambayo yatawasaidia kujitegemea katika maisha yao.
Kwa upande wake Grace Makenya ambaye ni mdhamini wa Chama alimshukuru Mama Kikwete kwa kuwatembelea na kusema kuwa watoto wengi ambao ni wanachama wa gilrs uides wameweza kufanya vizuri katika mitihani yao ya darasa la saba na wanawake walioolewa wameweza kuzitunza ndoa zao vizuri hii ni kutokana na mafunzo wanayowapatia.
Makenya alisema kuwa miradi waliyonayo ni jiko la kutumia mionzi ya jua, hosteli kwa shule za Sekondari za kutwa na mradi wa lishe bora kwa watoto wenye utapiamlo, afya ya uzazi na maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), mimba zisizotarajiwa kwa wasichana wadogo na utoaji wa elimu ya Ukimwi kwa jamii.
Chama hicho ambacho kimeenea Dunia nzima hapa nchini kilianza mwaka 1928 huku kikiwa na dira ya kuwa na wasichana ambao wanauelewa wa matukio ya kitaifa na ulimwengu, wenye kujiamini na kujitegemea na kuwa tayari kuhudumia jamii na wenye hamu ya kufanya kazi na watu wengine.
No comments:
Post a Comment