Monday, July 29, 2013

UKOO WATISHIWA KUTEKETEZWA KWA USHIRIKINA HUKO TABORA


Watu watatu wa ukoo mmoja wameuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na imani za kishirikina katika Wilaya ya Nzega Tabora, huku ujumbe mkali wa kuuawa kwa watu wengine ukiachwa katika Kijiji cha Nsanga.


Tukio hilo lilitokea katika kijiji hicho kilichopo Kata ya Ikindwa Nzega, Julai 25 mwaka huu, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Nzega Bituni Msangi alisema sababu ya mauaji hayo ni kukithiri kwa imani za kishirikina kwa baadhi ya wananchi wa kijiji hicho.



Aliwataja waliouawa kuwa ni Catherin Shija (65), Fransnc Kaliki (69) pamoja na Maria Kulwa (52) wote wakiwa ni wa ukoo mmoja wakiishi katika kijiji hicho.



Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho alisema watu wanaofanya mauaji hayo wanaishi nao, huku usiri mkubwa wa kuwataja kwenye vyombo vya dola ukiwa umetawala.



Alisema baada ya kuuawa vikongwe hao wa ukoo mmoja, waliotenda tukio hilo waliacha ujumbe mfupi wa barua katika kijiji hicho kuwa watu watatu wa kijiji hicho watauawa kwa kukatwakatwa mapanga muda wowote kuanzia sasa.



Ujumbe huo ulisema kuwa kutokana na watu hao kukaa mbali zoezi hilo limeshindikana kuuawa wote kwa pamoja na kuongeza kuwa ndani ya saa 24 watu hao watauawa.



Msangi akisoma ujumbe huo na kutaja majina yaliyokuwa yameandikwa kuwa ni Mwanamagazi, Mwanakizinga pamoja na mwanawe ambaye jina lake halikufahamika, wote wakiishi katika kijiji hicho wanatuhumiwa kwa ushirikina .



Aliwataka wananchi hao kutokuamini imani za kishirikina na macho mekundu kutokana na vikongwe wengi kufanya kazi za kijamii ikiwa ni pamoja na kutumia kuni za kupikia ambazo husababisha hali hiyo.


Alitaka doria za vitongoji kuimarishwa ikiwamo Sungusungu kulinda mazingira ya vijiji pamoja na kutambua watu wageni wanaoingia katika vijiji ili kuweza kupunguza mauaji hayo ya vikongwe.



Mkuu wa Polisi Wilaya, Yusuph Sarungi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa upelelezi mkali unaendelea wa kubaini wahalifu wa tukio hilo.

No comments:

Post a Comment