Thursday, September 12, 2013

Polisi mkoani Dodoma yashindwa kumfikisha mahakamani mbunge SUGU wa Mbeya mjini

JESHI la Polisi mkoani Dodoma limeshindwa kumpandisha kizimbani Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), kwa madai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Mbilinyi, maarufu kama ‘Sugu’ alifunguliwa jalada na jeshi hilo Ijumaa iliyopita, akidaiwa kumjeruhi jichoni askari wa Bunge, Koplo Nikwisa Nkisu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Wakili wake, Tundu Lissu, alisema kuwa hawakufikishwa mahakamani kama walivyotegemea kutokana na kuelezwa kuwa upelelzi haujakamilika.

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema kuwa baada ya mteja wake kuripoti kituoni aliambiwa kwamba upelelezi huo ukikamilika wataitwa ili kupewa maelezo ya hatua gani inafuata.

Alisema kitendo hicho cha polisi kuwaita bila kukamilisha upelelezi wao ni kuwapotezea muda.

“Nashangaa ni kwanini tunaitwa, tuliambiwa tufike hapa, lakini tulipokuja hapa hakuna jambo lolote la maana tuliloambiwa, badala yake wanasema tuendelee na shughuli zetu upelelezi haujakamilika na baada ya wiki mbili watatuambia kinachoendelea.

“Yaani, haya mambo yanayofanywa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi na Naibu wa Spika, Job Ndugai, ni ya ajabu sana. Tumeitwa kutoka mbali kote kwa ajili ya kuja hapa kuambiwa kuwa upelelzi haujakamilika,” alisema.

Aliongeza kuwa Sugu alitoka Mbeya huku naye akitoka huko alikokuwa kwa ajili ya kuja Dodoma lakini hakuna jambo lolote limefanyika, na kuhoji ni kwanini wasingearifiwa hata kwa simu.

Lissu alisema kuwa atashanga kama jeshi hilo litapeleka kesi hiyo mahakamani kwani kosa lenyewe lilifanyikia bungeni.
“Nitashangaa kama jambo hili litapelekwa mahakamani, kwani kwa mujibu wa kanuni, mbunge hatashitakiwa kwa jambo ambalo alilitenda akiwa katika maeneo ya Bunge.

“Mambo haya yalitokea tukiwa bungeni na huko kuna kinga ya mbunge. Mbunge akikosa anahukumiwa kwa mujibu wa kanuni, lakini kwa fikra na mashikinizo ya viongozi wa CCM wanataka kuvuruga na kufanya mambo kwa masilahi ya chama chao,” alisema.

Naye Sugu alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Ndugai ni cha kihuni na wala hakikuwa na misingi yoyote hadi kulazimisha askari wa Bunge kumpiga.

No comments:

Post a Comment