Tuesday, October 15, 2013

JAKAYA KIKWETE"TUMEWASHINDA MAADUI ZETU WALITAKA KUPANDIKIZA CHUKI"

Rais Jakaya Kikwete amesema maadui wote ambao walitaka kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi wamedhibitiwa .

Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake itaendelea kulinda amani ya nchi na maadui wote wanaohusika na kutaka kuvuruga nchi watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Kulikuwapo na upepo mbaya, lakini kwa sasa Tanzania ni shwari na tumemshinda adui,” alisema Rais Kikwete jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandamana na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru, mkoani Iringa.

Alisema katika siku za hivi karibuni, maadui wasioitakia mema Tanzania walikuwa na mkakati wa kuvuruga amani ya nchi, lakini Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola vimewadhibiti na nchi iko salama.

Rais Kikwete alisema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu inajua wazi kwamba nchi ikiingia kwenye mgawanyiko, mshikamano utavurugika na shughuli za maendeleo zitasimama.

Katiba Mpya

Rais Kikwete alisema mwaka 2014 ni mwaka wa kipekee kwa nchi kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.

Rais Kikwete alisisitiza kwamba Katiba Mpya ni lazima ikamilike mwakani kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa.

Vilevile, alisema mwakani Tanzania itasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na kuwarudishia Wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake.

“Pia tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wetu. Nawaomba Watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo hayo ili historia mpya ifunguliwe nchini.

“Wazanzibari waanze miaka mingine baada ya miaka hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya miaka hamsini na Katiba Mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema Kikwete.

Rais Kikwete alionya kuwa asingependa mchakato wa kupata Katiba Mpya uligawe taifa na kuleta mfarakano utakaovunja umoja wa kitaifa badala ya kuuimarisha.


“Tunataka tuwe na Katiba itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais Kikwete.
-Mwananchi

No comments:

Post a Comment