Tuesday, October 15, 2013

UFOO SARO"SIJAMBO NAENDELEA VIZURI

Hali ya mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro aliyejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi mbili juzi huko Kibamba, Dar es Salaam inazidi kuimarika na jana alizungumza na gazeti hili na kusema; “Sijambo, naendelea vizuri.”

Ufoo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hata hivyo, anazungumza kwa shida kutokana na kukabiliwa na maumivu baada ya kufanyiwa upasuaji juzi.

Mwandishi huyo amehamishiwa katika wodi ya upasuaji wa moyo huku kiongozi wa wodi hiyo, ambaye alikataa jina lake kuandikwa gazetini, akieleza kuwa walimhamishia huko ili apate muda zaidi wa kupumzika.

“Watu wanakuja kwa wingi kumjulia hali, tuliona tumhamishe ili apumzike,” alisema kiongozi huyo.

Kabla ya kupelekwa katika wodi hiyo, Ufoo alikuwa katika wodi ya Kibasila na baadaye alihamishiwa katika Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).

Ufoo alipigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi ambaye alijiua baadaye. Pia Mushi anatuhumiwa kumuua mama yake Ufoo, Anastazia Saro wakati wa tukio hilo.

Mazishi ya mama yake Ufoo yamepangwa kufanyika Ijumaa huko Machame mkoani Kilimanjaro.

Ufoo aongea kwa shida

Mara baada ya mwandishi wa gazeti hili jana kuingia

katika chumba alicholazwa Ufoo huku akisindikizwa na wauguzi watatu, mwandishi huyo alitoa mkono wake na kusema; “Njoo hapa unisalimie huku umenishika mkono.”

Huku akionyesha uchovu na kusikia maumivu, alizungumza kwa tabu na kusema; “Sijambo naendelea vizuri.”

Mara baada ya wauguzi hao kumweleza kuwa kati ya waandishi zaidi ya 30 waliofika kumjulia hali ni watatu tu ndiyo walioruhusiwa kumwona alitaka kujua ni kina nani waliobaki nje kwa kuhoji; “Nani hao wako nje.”

-Mwananchi