Monday, August 26, 2013

KANISA LACHOMWA MOTO JIJINI DAR

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Kati, Usharika wa Segerea Wilaya ya Ilala, limechomwa moto na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana. 


Tukio hilo lilitokea saa saba usiku, wakati waumini wa kanisa hilo wakiwa katika mkesha wa maombi ya maandalizi ya mkutano wa injili unaoanza leo.


Mchungaji wa kanisa hilo, Noah Kipingu alisema wakati wakiwa katika maombi ghafla walisikia sauti ya kitu kilichorushwa kutoka nje ya kanisa kikiambatana na moto, ambapo kilianguka madhabahuni na kuanza kuunguza baadhi ya vifaa vya kanisa.


“Tukiwa tumesimama mbele ya madhabahu kwa njia ya mduara ndipo nyuma ya madhabahu ukatokea mlipuko mkubwa kwa sauti ya kishindo, na moto ukatanda madhabahu,” alisema Kipingu na kuongeza kuwa:


“Katika namna ya kibinadamu hakuna aliyeweza kuvumilia, kila mtu alikimbia akitafuta namna ya kujiokoa.”


Kipingu alisema kuwa alipobaini kuwa ulikuwa ni moto wa mafuta aliwaambia waumini wake waingie ndani kwa ajili ya kuuzima, wakati wakiuzima moto huo walipata taarifa kuwa gari la Mchungaji, Toyota Cresta lenye namba za usajili T 482BAF lililokuwa nje ya kanisa lilikuwa likiwaka moto. 

“Baadhi ya waumini waliokuwa ndani walikwenda nje kushirikiana na mlinzi kuuzima moto huo, tunamshukuru Mungu kwamba matukio yote mawili tumeyashinda kwa uwezo wake,” alisema.


Kipingu alisema kuwa shambulizi hilo lilizua taharuki kubwa kwa waumini wake, na kwamba baadhi ya watu waliwaona watu wanne wakikimbia kutoka eneo la kanisa baada ya kutukio hilo.


Shukuru Thobias mmoja wa waumini waliokuwepo kanisani wakati tukio hilo likitokea, anasema aliona vitu kama mshale vikianguka madhabahuni na vilipodondoka vililipuka kama moto.


“Moto ulianza kuunguza Biblia na makapeti, ndipo tukaanza kukimbia kwenda nje kuchukua mchanga na kuanza kuuzima. 

"Baada ya hapo tulianza kukimbia huku wengine wakidondoka na kujeruhiwa kidogo miguuni. Niliporudi baadaye niligundua zilikuwa ni chupa tatu za bia zilizokuwa zimetengenezwa bomu la petroli,” alisema Thobias.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo hakuna mtu aliyepoteza maisha na kulitaja kuwa ni jaribio la kiharifu lililoshindwa.


“Hakuna mtu aliyepoteza maisha, lilikuwa jaribio ambalo halikufanikiwa. Wakati tukio linatokea waumini walikuwa kanisani kwa hiyo waliwahi kuuzima moto kabla haujaleta madhara,” alisema Kova.



Matukio ya makanisa kuchomwa moto
Mei 26, 2012, Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililopo Mtaa wa Kariakoo mjini Unguja, lilichomwa moto usiku na watu wasiofahamika.

No comments:

Post a Comment