Thursday, April 10, 2014

SIMULIZI TAMU YA WEMA SEPETU-5

Wema Sepetu 'Madam'.

VIPI KUHUSU HARTMANN?
Mwandishi: Iliwahi kusemekana kuwa kuna wakati uliangukia kwenye penzi la mjasiriamali anaitwa Hartmann Mbilinyi, ni kweli?

Wema: Yale yalikuwa maneno ya watu. Unajua Hartmann nilikuwa nafanya naye kazi za filamu, wakati ule alikuwa na kampuni yake inaitwa Hartmann Production, watu wakadhani ‘nadate’ naye, si kweli bwana.

Mwandishi: Wema unaweza kutuambia mwanaume gani alifuata baada ya wewe kuachana na Diamond akawa na Jokate?
Sasa endelea….

Wema: Baada ya Diamond nilipenda sana kuishi mwenyewe kwani sikuwa na hamu ya kuwa na mpenzi. Nilichoshwa sana.

AKUMBUKA MACHUNGU YA DIAMOND KUKATAA KUPOKEA FEDHA ZAKE JUKWAANI
Mwandishi: Kuna mwaka uliwahi kuhudhuria shoo ya Diamond pale Mlimani City, tayari akiwa na Jokate rasmi, ukaenda kumtuza pesa jukwaani akazikataa, ulijisikiaje?

Wema: Sitaki kukumbuka. Ilikuwa mbaya sana. Unajua nilikwenda kama shabiki lakini yeye akachukulia vingine, iliniuma sana. Lakini nilisema yote maisha.

“Nisingeweza kumfuata Diamond kwa lengo lingine wakati najua alikuwa na Jokate.
“Hata nilipofika nyumbani bado akili zangu zilikuwa zikirudia lile tukio mara kwa mara. Hapo ujue ni jinsi gani niliumia ila nasema na watu wajue kwamba sikwenda kwa nia nyingine zaidi ya kutuza kama mashabiki wengine tu.

“Kuna watu walinishauri kwamba ningefanya fujo palepale ukumbini lakini hilo nililiona ni wazo baya, Diamond hakujua kwamba napenda muziki wake hata kama yeye tuliachana akawa na Jokate.
“Jokate mwenyewe kwa sasa tupo sawa kabisa, tulikutana Arusha tukayaongea, anajua kwa sasa nimerudiana na Diamond, imebidi akubali matokeo kama mimi nilivyo yakubali matokeo wakati ule.”

KUHUSU KIGOGO WA IKULU
Mwandishi: Vipi ukajikuta umeangukia kwa Clement wa Ikulu?
Wema: Yule alikuja baada ya kuwa singo. Nilimkubali kwa sababu kwa wakati ule sikuona kipingamizi cha mimi na yeye kuwa wote, ni mwanaume anayejua kulea, kupenda.

Mwandishi: Ulijua ni mume wa mtu wakati mnaanzana?
Wema: Hapana, lakini nadhani kwa sababu hatukulizungumzia hilo zaidi ya uhusiano wangu na wake. Na alijua nilikuwa na Diamond, tukaachana.

Mwandishi: Unaweza kueleza kidogo maisha yenu ya kimapenzi?
Wema: Kwa yule tuachane naye.
Mwandishi: Kwa nini mliachana?

Wema: Ilitokea, ikawa hivyo.
Mwandishi: Inadaiwa yeye ndiye aliyekupangia ile nyumba na kukununulia kila kitu cha ndani, ni kweli?
Wema: Nasisitiza yule tumwache.

Mwandishi: Ni kweli ni mfanyakazi wa Ikulu?
Wema: (akionesha kukasirika) lakini si nimeshasema yule tumwache, mbona bado unaniuliza maswali kuhusu yeye au unapenda tufikie mwisho wa mahojiano yetu?

Mwandishi: Oke, kuna siku za furaha na siku za majonzi. Ni siku gani iliwahi kuwa ya furaha kwako na majonzi?
Wema: Siku Diamond aliponivisha pete ya uchumba pale Maisha Club. Nililia kwa furaha.
“Siku ambayo nilikosa furaha ikawa ya majonzi ni pale baba yangu mzazi (marehemu Isaac Sepetu) alipofariki dunia.” 

KUHUSU MKOROGO
Mwandishi: Wema umekuwa ukidai mkorogo uliharibu ngozi yako, ukatumia fedha nyingi kurekebisha ngozi. Lakini mbona upo vilevile?
Wema: Hapana, mimi ndiyo najijua, nilivyokuwa kabla na sasa. Ngozi yangu iliharibika sana kwa sasa iko sawa kabisa na sirudii tena kutumia mkorogo.

KURUDIANA NA DIAMOND KULIVYOTOKEA
Mwandishi: Sasa ilikuwaje ukarudiana na Diamond?

Itaendelea wiki ijayo.